Pezeshkian: Uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na Marekani ufuatiliwe kisheria kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140196-pezeshkian_uharibifu_wa_miundombinu_uliosababishwa_na_marekani_ufuatiliwe_kisheria_kimataifa
Rais Masoud Pezeshkian amelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya miundombinu ya usafiri ya Iran akiyataja kuwa ni "uhalifu wa kivita," na kutaka hatua za kisheria za kimataifa zichukuliwe dhidi ya uharibifu uliosababishwa na nchi hiyo kwenye vituo vya mpakani, vituo vya forodha na mitandao ya usafirishaji.
(last modified 2026-07-27T03:59:08+00:00 )
Jul 27, 2026 03:57 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian
    Rais Masoud Pezeshkian

Rais Masoud Pezeshkian amelaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya miundombinu ya usafiri ya Iran akiyataja kuwa ni "uhalifu wa kivita," na kutaka hatua za kisheria za kimataifa zichukuliwe dhidi ya uharibifu uliosababishwa na nchi hiyo kwenye vituo vya mpakani, vituo vya forodha na mitandao ya usafirishaji.

Akizungumza na maafisa wakuu wa Wizara ya Barabara na Maendeleo ya Mijini jana Jumapili, Rais Pezeshkian alipitia tathmini ya hivi karibuni ya uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya kichokozi ya Marekani kwenye sekta ya uchukuzi hapa nchini na hatua zilizochukuliwa ili kudumisha huduma muhimu katika sekta hiyo.

Rais Pezeshkian amechunguza ripoti zinazohusu uharibifu wa vituo vya mpakani, vifaa vya forodha, bandari, madaraja, barabara kuu, mitandao ya reli na miundombinu mingine ya kimkakati ya usafiri, kabla ya kutoa maagizo ya kuharakisha ujenzi upya na kuazisha njia mbadala za usafirishaji.

Akiyataja mashambulizi hayo kuwa ni "ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na uhalifu wa kivita," Pezeshkian amesisitiza kwamba uharibifu uliosababishwa kwenye vituo vya mpakani vya Iran, vifaa vya forodha na miundombinu ya usafiri wa nchi kavu, reli, baharini na anga lazima ufuatiliwe kupitia vyombo vya kisheria vya kimataifa.

Amewapongeza wafanyakazi wa Wizara ya Barabara na Maendeleo ya Mijini kwa kudumisha huduma muhimu licha ya mashambulizi hayo ya Marekani na kusema: "Kuendelea kutoa huduma, uthabiti wa mtandao wa usafirishaji na kuzuia kuyumba huduma za barabara, reli, anga na bandari kunaonyesha kujitolea, ufanisi na ari ya kutoa huduma ya wafanyakazi wa wizara hii."

"Kwa moyo huu, pamoja na juhudi za dhati za matawi yote ya serikali na msaada wa wananchi, njama zote za adui zinazolenga kuvuruga huduma na miundombinu ya nchi zitafeli," ameongeza Rais Masoud Pezeshkian.

Katika wimbi jipya la mashambulizi ya kijeshi ya hivi karibuni ya Marekani, Washington ililenga vituo kadhaa vya usafirishaji wa raia katika maeneo ya kusini mwa Iran.

Iran imekuwa ikijibu kwa kuvurumisha makombora na ndege zisizo na rubani kwenye vituo na kambi za Marekani na Israel katika eneo la Asia Magharibi, sambamba na kufunga Lango-Bahari la Hormuz.