Baqaei: Hatua hatari za kukurupuka za Ukraine zitapewa majibu muwafaka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140214-baqaei_hatua_hatari_za_kukurupuka_za_ukraine_zitapewa_majibu_muwafaka
Shambulio la Ukraine dhidi ya meli ya Iran lilikuwa kinyume cha sheria, limekiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa na ni kitendo hatari cha kichokozi.
(last modified 2026-07-28T03:47:26+00:00 )
Jul 28, 2026 03:45 UTC
  • Esmaeil Baqaei
    Esmaeil Baqaei

Shambulio la Ukraine dhidi ya meli ya Iran lilikuwa kinyume cha sheria, limekiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa na ni kitendo hatari cha kichokozi.

Hayo yameelezwa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baqaei ambaye ameongeza kuwa hatua hiyo haitapita bila jibu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ambaye alikuwa katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari jana Jumatatu mjini Tehran pia aliashiria mazishi ya baadhi ya watoto wa shule ya Minab yalilofanyika tarehe 22 mwezi huu wa Julai, ambapo wananchi wa Iran walizika viungo na sehemu za miili ya baadhi ya wavulana na wasichana wadogo wa Kiirani waliouawa kinyama katika shambulizi la Marekani; tukio ambalo ni nadra kushuhudiwa katika historia.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari jana Jumatatu, Esmaeil Baqaei alimhutubu Kaja Kallas, Makamu Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, ambaye mara kwa mara amekuwa akidai kuwa ana wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Iran kwa kuhoji: Je hawa watoto waliouwa si Wairani? Si raia wasio na hatia?

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia alijibu swali la mwandishi wa habari wa shirika la habari la IRNA kuhusu shambulio la hivi karibuni la Ukraine dhidi ya meli ya Iran ambalo liliuwa shahidi na kuwajeruhi raia kadhaa wa Iran pamoja na hatua za kidiplomasia zilizofuata, ikiwemo taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, kuitwa Kaimu Balozi wa Ukraine katika Wizara ya Mambo ya Nje na mazungumzo ya simu kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Kallas, na kusema: Bila shaka, wale wanaojitambua kama waungaji mkono wa serikali ya Ukraine wanapasa kuwajibika kuhusu suala hili.