Jeshi la Sudan ladai kudhibiti barabara kuu inayounganisha Khartoum na El-Obeid
-
Jeshi la Sudan
Jeshi la Sudan limetangaza kuwa limerejesha udhibiti kamili wa barabara kuu inayounganisha mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum, na El-Obeid, mji ambao umekuwa ukizingirwa na kundi la wanamgambo Rapid Support Forces (RSF).
Kutekwa barabara kuu ya Al Sadarat siku ya Jumapili kutalisaidia jeshi la Sudan kusafirisha askari, silaha, mafuta na vifaa, na pia kutazuia jaribio la RSF la kutaka kuuteka mji wa El-Obeid ambao ni makao makuu ya jimbo la Kordofan Kaskazini.
Takriban watu nusu milioni wamekwama katika mji huo, na Umoja wa Mataifa umeonya kuhusu janga la binadamu, huku wakazi wake wakikabiliwa na mashambulizi makali ya ndege zisizo na rubani ya wanamgambo wa RSF.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, jeshi la Sudan lilisema kuwa limeteka tena miji iliyopo kati ya Khartoum na El-Obeid kufuatia mapigano makali ya siku mbili dhidi ya kundi la RSF, ambalo lilikuwa likidhibiti barabara hiyo kuu.
Mashambulizi hayo yalikuwa hatua kuu ya kwanza ya jeshi la Sudan dhidi ya kikosi hicho cha waasi katika kipindi cha miezi kadhaa ya karibuni.
Jeshi la Sudan limeeleza kuwa vikosi vyake vimerejesha udhibiti wa maeneo ya Um Qurfa na Jarigakh kufuatia operesheni zilizosababisha "hasara kubwa ya maisha na vifaa kwa wanamgambo wa RSF na kuwalazimu kukimbia".
"Kwa ushindi huu, askari wetu wamedhibiti njia ya usafirishaji ya Omdurman-Al-Abyd," imeongeza taarifa ya jeshi la Sudan ikiashiria barabara kuu ya Al Sadarat.