Baghaei: Marekani imesaliti diplomasia kwa mara ya tatu
-
Baghaei: Marekani imesaliti diplomasia kwa mara ya tatu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema kuwa Marekani imeisaliti diplomasia kwa mara ya tatu, akieleza kuwa hatua za Washington zimeendelea kudhoofisha juhudi za kutatua migogoro kupitia mazungumzo.
Baghaei ameeleza kuwa, badala ya kuzingatia njia za kidiplomasia na kuheshimu ahadi zake, Marekani imechukua hatua ambazo, kwa mujibu wake, zinapingana na misingi ya diplomasia na zinachangia kuongezeka kwa mvutano katika eneo.
Aidha, alisisitiza kuwa Iran itaendelea kutetea maslahi yake ya kitaifa na kwamba mafanikio ya diplomasia yanategemea kuheshimiwa kwa ahadi na kuzingatiwa kwa sheria za kimataifa na pande zote zinazohusika.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ORF cha Austria na kubainisha kwamba, makubaliano ya Islamabad si hati ndefu wala yenye utata, bali ni waraka mfupi wa maelewano wenye vipengele 14.
Baghaei amesema kuwa, dunia ilikuwa na matarajio kwamba angalau safari hii Marekani ingetimiza ahadi zake. Hata hivyo, hatua zilizochukuliwa na Washington zilikiuka kwa uwazi na kwa kiwango kikubwa vipengele mbalimbali vya makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, hatua hiyo inaashiria kuwa Marekani "imeisaliti diplomasia kwa mara ya tatu," akisisitiza kwamba ukiukaji wa ahadi za kimataifa unadhoofisha juhudi za kutatua migogoro kupitia mazungumzo na diplomasia.
Esmaeil Baghaei amesema Iran imekuwa ikihakikisha usalama wa Lango Bahari la Hormuz na Ghuba ya Uajemi kwa nia njema kwa miongo kadhaa, licha ya kukabiliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi kwa miaka mingi.
Akijibu swali kuhusu chanzo cha misukosuko ya hivi karibuni katika lango hilo, Baghaei alikanusha madai yoyote yanayoihusisha Iran na matukio hayo. Amesema hali ya sasa ya sintofahamu ni matokeo ya moja kwa moja ya mashambulizi yaliyofanywa na Marekani na Israel tangu tarehe 28 Februari, na kwamba, jamii ya kimataifa inapaswa kutambua kwamba, Iran haipaswi kulaumiwa kwa matokeo ya hatua zisizo sahihi za mataifa mengine.