Putin: Maadui wa Russia wamejielekeza katika mbinu za wazi za kigaidi
-
Rais wa Vladimir Putin wa Russia
Rais wa Vladimir Putin wa Russia amesema kuwa maadui wa nchi hiyo wameamua kutumia mbinu za wazi za kigaidi, na kwamba Moscow itatimiza malengo yake yote ya kijeshi katika vita vya Ukraine na iko tayari kutoa jibu kwa hatua yoyote ya uhasama.
Rais Putin alisema jana katika mkutano na wawakilishi Bunge la Russia (Duma) kwamba wapinzani na maadui wa Russia baada ya kushindwa kutoa kipigo kwa nchi hiyo katika uwanja wa vita sasa wameamua kutumia vitendo vya wazi vya kigaidi dhidi ya watu wa Russia.
Putin amesema: "Wale walioshindwa kuishinda Russia vitani sasa wameamua kutumia mbinu za wazi za kigaidi katika vita vyao dhidi ya watu wetu; hata hivyo, wananchi wa Russia kamwe hawatasambaratishwa na nguvu ya yeyote."
Rais wa Russia pia amesisitiza kuwa nchi hiyo itatimiza malengo yake yote ya kijeshi katika vita dhidi ya Ukraine, na kwamba serikali ya Moscow ikishirikiana na taasisi mbalimbali, na iko tayari kikamilifu kukabiliana na hatua yoyote ya uhasama.
Mwishoni mwa mkutano wake na vyombo vya habari Rais Putin amesema wananchi wa Russia wako tayari kulinda nchi na kwamba wanaweza kutoa jibu madhubuti dhidi ya hatua yoyote ya uhasama kwa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa jamii za nchi hiyo.