Je, Marekani imefikia mkwamo wa kimkakati katika mgogoro wake na Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140200-je_marekani_imefikia_mkwamo_wa_kimkakati_katika_mgogoro_wake_na_iran
Wachambuzi wengi mashuhuri wa Marekani wanaonya kwamba Washington inatembea kwenye njia ya mgogoro na Iran ambayo si lazima ifanikiwe kisiasa au kistratijia. Wanaamini kwamba changamoto kuu inayoikabili Marekani kwa sasa si kuanzisha vita, bali ni kutafuta njia ya kujiondoa kwenye mkwamo unaozidi kuongezeka siku hadi siku.
(last modified 2026-07-27T07:12:45+00:00 )
Jul 27, 2026 07:10 UTC
  • Je, Marekani imefikia mkwamo wa kimkakati katika mgogoro wake na Iran?

Wachambuzi wengi mashuhuri wa Marekani wanaonya kwamba Washington inatembea kwenye njia ya mgogoro na Iran ambayo si lazima ifanikiwe kisiasa au kistratijia. Wanaamini kwamba changamoto kuu inayoikabili Marekani kwa sasa si kuanzisha vita, bali ni kutafuta njia ya kujiondoa kwenye mkwamo unaozidi kuongezeka siku hadi siku.

"Dunia bado haijaona ukubwa kamili wa nguvu ya Iran." Kauli hii ya Scott Ritter, mkaguzi wa zamani wa silaha wa Umoja wa Mataifa na afisa wa zamani wa kijasusi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, inatumika kama onyo kuhusu kufikia kikomo nguvu za Marekani. Katikati ya uchokozi unaoendelea wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran, wachambuzi mashuhuri wa Marekani wenye mitazamo tofauti, kuanzia Scott Ritter hadi John Mearsheimer na Tucker Carlson wamefikia hitimisho moja nalo ni kuwa, Washington imeingia kwenye vita ambavyo ilikuwa rahisi kuvianzisha lakini ni vigumu sana kuvimaliza.

Katika fasihi ya kimkakati, kuna tofauti ya kimsingi kati ya "ushindi wa mbinu" na "mafanikio ya kimkakati." Hata kama Marekani inaweza kutumia ubora wake wa anga kushambulia miundombinu maalum au malengo ya kijeshi, lakini hili halina maana ya kuafikiwa malengo ya kisiasa. John Mearsheimer, mwananadharia mkuu wa shule ya uhalisia, anafafanua zaidi suala hili kwa kusema: "Nguvu ya kijeshi huwa na maana tu pale inapoweza kubadilisha nia ya kisiasa ya adui. Ikiwa mabadiliko kama hayo hayatatokea, hata operesheni kubwa zaidi za kijeshi zitashindwa kufikia ushindi wa kimkakati."

Scott Ritter anaelezea uhalisia huohuo kwa mtazamo wa kiutendaji. Anahoji kuwa iwapo vita vitaongezeka makali, Marekani haitakabiliwa tu na uhaba wa rasilimali na kudhoofika kwa uwezo wake wa kivita, bali pia itapoteza fursa yake muhimu zaidi ambayo ni uhuru wa kuchukua hatua yoyote inayotaka katika eneo. Kwa mtazamo wake, mapigano yoyote ya nchi kavu na kupanuliwa kijiografia eneo la mgogoro kutaiongezea Washington gharama zinazopindukia makadirio ya awali. Kwa msingi huo, suala la msingi si uwezo wa kuanzisha vita, bali ni uwezo wa kudhibiti matokeo yake.

Tathmini hiyo hiyo inaonekana pia katika uchambuzi uliofanywa na gazeti la Los Angeles Times. Gazeti ambalo kwa kuzingatia kurefuka vita, linachambua namna Trump alivyonasa katika kinamasi kile kile cha "vita visivyo na mwisho" ambavyo alikuwa ameahidi kwa muda mrefu kuvimaliza. Kuongezeka kwa idadi ya wahanga, mzunguko wa mashambulizi ya kulipiza kisasi, na kukosekana ufafanuzi wa wazi kuhusu maana halisi ya "ushindi," vyote vinaashiria kuwa mzozo huu umevuka hatua ya operesheni za muda mfupi na kugeuka kuwa mgogoro wa kimkakati.

Katika muktadha huu, Tucker Carlson, shakhsia mashuhuri katika vyombo vya habari vya mrengo wa kihafidhina nchini Marekani, anaangazia kipengele kingine muhimu cha vita hivi: Mgogoro wa uhalali wa kisiasa. Anahoji kuwa kuingia Marekani katika vita dhidi ya Iran si tu kwamba kunakinzana wazi na ahadi za kampeni za Trump za kuepuka migogoro ya nje, bali pia kunaiacha bila mkakati wowote wa wazi wa kujinasua kutoka kwenye mgogoro uliopo.

Swali rahisi lakini muhimu la Carlson ni hili: Ikiwa lengo la vita halijafikiwa na njia ya kuvimaliza bado haieleweki, je, kuendelea kwa vita kutakuwa na faida gani?

Maoni ya Ritter, Mearsheimer, na Carlson yanakutana kwenye ukosoaji wa dhana potofu ya muda mrefu katika sera za kigeni za Marekani kwamba nguvu na ubora wa kijeshi pekee unaweza kubadilisha milinganyo ya kisiasa duniani. Uzoefu wa Afghanistan, Iraq, na katika muktadha huu, vita vya Iran vimeonyesha kwa mara nyingine kwamba nguvu ya moto pekee haiwezi kuchukua nafasi ya mkakati wa kisiasa. Taifa lenye ukubwa wa kijiografia, uwezo madhubuti wa kijeshi, nguvu ya makombora na uwezo wa kumtwisha adui gharama kubwa haliwezi kuondolewa kirahisi kwenye mlingano wa nguvu kupitia mashambulizi ya anga pekee.

Mbali na hayo, vita vya muda mrefu huwa na matokeo ambayo huenea zaidi ya mipaka ya uwanja wa vita. Kupanda kwa gharama za kijeshi, matatizo katika uchumi wa Marekani, kupungua kwa hifadhi ya silaha, kuhatarishwa usalama wa njia za nishati na kuongezeka migawanyiko ya kisiasa ya ndani, yote hayo ni sehemu ya gharama za vita ambayo inazidi kuwa vigumu kuidhamini kila siku inayopita.

Katika mazingira haya, hata kama Marekani itaendelea kuwa na uwezo wa kuendesha operesheni za kijeshi kwa sasa, lakini swali la msingi linabakia kuwa, je, operesheni hizo zinaweza kutoa matokeo ya kisiasa yanayotarajiwa na watawala wa Washington?

Ukweli ni kwamba kushindwa katika vita siku zote hakuna maana ya kushindwa kwenye uwanja wa vita tu. Wakati mwingine, kushindwa hutokea wakati nguvu kuu, licha ya kuwa na ubora wa kijeshi, inaposhindwa kufikia malengo yake yaliyotangazwa rasmi na hatimaye kulazimika kurudi kwenye njia ya diplomasia bila kupata matokeo yaliyotarajiwa. Uchambuzi wa mitazamo ya Scott Ritter, John Mearsheimer na Tucker Carlson unaonyesha kuwa kwa hasa hii ndiyo hofu yao kuu: kwamba Marekani inaendelea kunasa zaidi katika mkwamo wa kimkakati, hali ambayo kuondokana nayo, kunategemea zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kuchukuliwa maamuzi ya kisiasa badala ya mabomu ya ziada.