Rais Pezeshkian: Israel ilijaribu kuniua, siogopi kifo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128068-rais_pezeshkian_israel_ilijaribu_kuniua_siogopi_kifo
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa utawala haramu wa Israel ulitekeleza jaribio la kumuua wakati wa vita hivi karibuni. Aidha amesisitiza kuwa Iran “haina tatizo” kurejea kwenye mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia, lakini anasisitiza kuwa lazima kuwe na dhamana kwamba Israel haitafanya tena shambulio wakati wa mazungumzo ya kidiplomasia, kama ilivyofanya mwezi uliopita.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jul 08, 2025 04:24 UTC
  • Rais Masoud Pezeshkian wa Iran
    Rais Masoud Pezeshkian wa Iran

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema kuwa utawala haramu wa Israel ulitekeleza jaribio la kumuua wakati wa vita hivi karibuni. Aidha amesisitiza kuwa Iran “haina tatizo” kurejea kwenye mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia, lakini anasisitiza kuwa lazima kuwe na dhamana kwamba Israel haitafanya tena shambulio wakati wa mazungumzo ya kidiplomasia, kama ilivyofanya mwezi uliopita.

Katika mahojiano ya mtandaoni na mchambuzi wa kisiasa wa Marekani, Tucker Carlson, yaliyotangazwa Jumatatu, Rais Pezeshkian aliongeza kuwa kurejea kwenye meza ya mazungumzo kunahitaji mazingira ya kuaminiana:
Mnamo Juni 13, utawala wa Israel ulianzisha mashambulizi ya kichochezi dhidi ya Iran, na kuwaua makamanda waandamizi wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, pamoja na raia wa kawaida wakiwemo wanawake na watoto.

Siku ya Juni 22, Marekani nayo iliingia rasmi vitani dhidi ya Iran kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia nchini, hatua ambayo Iran imeitaja kuwa ni ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT).

Mashambulizi hayo yalifanyika wakati Iran na Marekani zilikuwa tayari zimefanya duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, yakisimamiwa na Oman, tangu Aprili, na walikuwa wakijiandaa kwa duru mpya ya mazungumzo mjini Muscat mnamo Juni 15.

Katika mahojiano hayo, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran haijawahi kuanzisha vita na haitamani vita viendelee. Alikemea kampeni ya upotoshaji ya Israel dhidi ya Iran ambayo imekuwepo kwa miongo kadhaa na kusema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amekuwa akieneza uongo kwamba Iran inatafuta silaha za nyuklia.

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa: “Hatujawahi kufuatilia utengenezaji wa silaha za nyuklia, hatufanyi hivyo sasa, na hatutawahi kufanya hivyo.” Aidha ameashiria  fatwa ya  Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kuhusu uharamu wa silaha za nyuklia.

Pia amesisitiza kuwa Iran imekuwa ikishirikiana kikamilifu na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), lakini akasikitika kuwa mwenendo wa hivi karibuni wa shirika hilo umevuruga ushirikiano huo.

Katika sehemu nyingine ya mahojiano, Rais Pezeshkian amefichua kuwa Israel ilijaribu kumuua wakati wa siku 12 za mashambulizi dhidi ya Iran.

Amesisitiza kuwa haogopi kifo na kusema: “Tuko tayari kuilinda nchi yetu, uhuru wetu, na ardhi yetu hadi pumzi ya mwisho. Hatuogopi kifo."

Amefafanua kuwa jaribio hilo la kumuua lilifanywa na Israel, si Marekani, na kwamba yeye pamoja na maafisa wengine waandamizi walikuwa kwenye kikao cha ndani wakati jengo walilokuwemo liliposhambuliwa.