Katiba DRC: Muungano wa upinzani wa C64 waanza tena mvutano na serikali
Mvutano wa kisiasa umeibuka tena katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya muda wa mwisho uliotolewa na wapinzani kumalizika siku ya Jumamosi, Agosti 15.
Muungano huo wa upinzani ulikuwa umempatia Rais Félix Tshisekedi muda wa hadi kufikia juzi Jumamosi kuitisha mazungumzo ya kitaifa yanayojumuisha mirengo yote.
Muungano huo wa upinzani wa C64, unaowajumuisha Martin Fayulu, Moïse Katumbi, Delly Sesanga, Jean-Marc Kabund, na Matata Ponyo ambao unapinga mabadiliko yoyote ya katiba, ulikutana Kinshasa ili kuanzisha upya uhamasishaji wake dhidi ya mabadiliko yaliyopendekezwa.
Lengo la mkutano wa C64, muungano wa upinzani nchini DRC, uliofanyika Jumamosi ya juzi Agosti 15, mjini Kinshasa, lilikuwa kutathmini ahadi zilizotolewa na serikali kwa mazungumzo jumuishi, pamoja na hatua za kupunguza mvutano zilizotekelezwa tangu mkutano wa Julai 17 kati ya Félix Tshisekedi na viongozi wa kidini ambazo wanasema hazitoshi.
Hapo awali, upinzani uliahirisha maandamano yao mjini Kinshasa kufuatia upatanishi wa viongozi wa dini (CENCO na ECC) ili kutoa nafasi kwa mchakato wa mazungumzo.
Haya hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekataa kushinikizwa na kueleza kuwa ratiba ya rais haiongozwi na vitisho vya makataa kutoka kwa wanasiasa.
Viongozi wakuu wa upinzani walikutana tarehe 15 Agosti kupanga mikakati mipya baada ya kupita tarehe hiyo bila utekelezaji wowote wa kuitishwa mazungumzo hayo ya kitaifa.