Iran: Trump anaongopa kudai kuwa tumeomba tufanye mazungumzo
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekanusha vikali matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump kwamba Tehran imeomba kufanyike mazungumzo, ikiikashifu Washington kwa kubuni madai yasiyo na msingi ili kuficha kushindwa kwake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei alisema jana Jumanne kwamba, hakuna ombi lolote la kufanya mazungumzo lililowasilishwa na Jamhuri ya Kiislamu kwa Marekani.
Amepuuzilia mbali matamshi hayo ya Trump na kuyataja kama jaribio la kutapatapa la kujaribu kuonyesha Marekani ina nguvu, katika hali ambayo itibari ya Washington inaendelea kuporomoka
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, "Kutoka kwa upande wetu, hakuna ombi la mkutano ambalo limetolewa kwa upande wa Marekani."
Trump siku ya Jumatatu alidai wakati wa mkutano na waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwamba Washington imepanga tarehe ya mazungumzo na Iran; na kwamba maafisa wa Iran walikuwa na hamu ya kuzungumza.
Kadhalika Rais wa Marekani alikariri madai yasiyo na msingi kuhusu shughuli za nyuklia za Iran. "Nadhani wanataka kukutana nasi ili kufikia amani," alibwabwaja Trump.
Trump alienda mbali zaidi, na kudai kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ulikuwa umesambaratisha kabisa na kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki umethibitisha kuharibiwa kwa eneo linalodaiwa kushambuliwa.
"Natumai vita kati ya Israel na Iran vimekwisha. Tutakuwa na mkutano na Iran na kuona nini kitatokea," Trump aliendelea kudai katika mkutano wake wa Netanyahu.