Jeshi la Israel lakiri askari wake 5 wameangamizwa, 14 wamejeruhiwa Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128076-jeshi_la_israel_lakiri_askari_wake_5_wameangamizwa_14_wamejeruhiwa_ghaza
Jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limetangaza kuwa askari wake watano wameuawa na wengine 14 wamejeruhiwa katika mapigano kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Jul 08, 2025 08:52 UTC
  • Jeshi la Israel lakiri askari wake 5 wameangamizwa, 14 wamejeruhiwa Ghaza

Jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel limetangaza kuwa askari wake watano wameuawa na wengine 14 wamejeruhiwa katika mapigano kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Taarifa iliyotolewa na jeshi hilo la kizayuni imesema: "askari watano wa batalioni ya Netzah Yehuda ya Brigedi ya Kfir waliuawa Jumatatu jioni katika mapigano kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza, na wengine 14 walijeruhiwa, wakiwemo wawili waliojeruhiwa vibaya".

Redio ya Jeshi la utawala wa kizayuni imeripoti kuwa tukio hilo lilitokea wakati askari wa doria ya miguu kutoka Kikosi cha Netzah Yehuda walipokuwa wakivuka mji wa Beit Hanoun.

Mtangazaji wa redio hiyo amesema: "askari hao wa kivita walipigwa na bomu lililotegwa kando ya barabara wakati wa operesheni za ardhini huko Beit Hanoun. Wanajeshi hao walikuwa wakitembea kwa miguu, na hawakuwemo ndani ya gari".

Abu Obaida, msemaji wa Brigedi za Izzuddinul-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, HAMAS, amesema "operesheni tata ya Beit Hanoun" iliyofanywa na wapiganaji Jumatatu jioni ni "pigo la ziada kwa haiba tete ya jeshi la Israel," na akatishia "kuwakamata mateka wanajeshi zaidi" hapo baadaye.

Msemaji wa Hamas amesisitiza kwa kusema: "uthabiti wa Wapalestina na ushujaa wa Muqawama unatengeneza taswira ya awamu inayofuata," akiongeza kwamba "uamuzi wa kipumbavu zaidi ambao Netanyahu anaweza kuchukua utakuwa ni wa kuweka majeshi yake ndani" ya Ukanda wa Ghaza.../