Israel inataka kuanzisha tena vita, Iran iko kwenye hali ya utayari kamili
Chanzo kimoja cha habari cha Iran kimeiambia chaneli ya Press TV kwamba utawala wa kizayuni wa Israel unataka vita viendelee na Rais wa Marekani Donald Trump anaonekana kuunga mkono suala hilo.
Chanzo hicho, ambacho kimezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kimesema, Iran inautathmini mkutano kati ya waziri mkuu wa utawala wa kizayuni Benjamin Netanyahu na Trump kwamba hautakuwa tofauti na mashauriano yao waliyofanya kabla ya vita vya siku 12.
"Utawala [wa Israeli] unataka vita, na tuna shaka kama Trump atapinga. Sisi pia tuko katika hali ya utayari kamili," kimebainisha chanzo hicho.
Chanzo hicho kimeongezea kueleza kwamba, Iran inaichukulia mikutano yote hiyo "kuwa ni ya hila" kwa sababu kila kitu kimeshaafikiwa tokea mapema.
Kikiashiria ombi la hivi karibuni la Marekani la kutaka kufanya mazungumzo na Iran, chanzo hicho kimesema, "ikiwa Trump anaamini kwamba baada ya kufanya shambulio la kijeshi dhidi ya mpango wetu wa nyuklia, tutaamini kufikia makubaliano ya kidiplomasia na wao, basi si mfanya mapatano mzuri."
Kwa mujibu wa chanzo hicho, "katika mazingira ya wakati wa vita, hakuna fursa ya kufikia amani. Ni mara baada ya kuivuka awamu hii ndipo tunaweza kufikiria amani."
Katika vita vya kulazimishwa vya Siku 12 vilivyoanzishwa Juni 13 na utawala haramu wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ulimwengu ulishuhudia uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na utawala huo wa kijinai huku ukipewa msukumo na uungaji mkono mkubwa wa kijeshi na Marekani.
Hata hivyo, katika jibu na mapigo makali yaliyofuata mara baada ya uvamizi huo, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilifanya mashambulizi yaliyolenga shabaha kwa umakini wa kiwango cha juu na kuviteketeza vituo muhimu vya nyuklia, vya kijeshi na vya miundomsingi ya viwanda ya utawala dhalimu wa Kizayuni.../