Russia yatoa mjibizo kwa muhula wa siku 50 iliopewa na Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128378
Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema, Russia inahitaji muda kutathmini kitisho alichotoa Rais wa Marekani Donald Trump cha kuwawekea vikwazo vikali washirika wa kibiashara wa Moscow ikiwa mzozo wa Ukraine hautatatuliwa ndani ya siku 50.
(last modified 2025-07-19T08:58:23+00:00 )
Jul 16, 2025 06:44 UTC
  • Russia yatoa mjibizo kwa muhula wa siku 50 iliopewa na Trump

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema, Russia inahitaji muda kutathmini kitisho alichotoa Rais wa Marekani Donald Trump cha kuwawekea vikwazo vikali washirika wa kibiashara wa Moscow ikiwa mzozo wa Ukraine hautatatuliwa ndani ya siku 50.

Siku ya Jumatatu, Trump alisema "hana furaha hata kidogo" kwa sababu ya Russia, akionya kuweka ushuru "mkali" wa hadi 100% ikiwa hazitapigwa hatua haraka katika diplomasia. Pamoja na hayo, rais huyo wa Marekani aliendelea kuacha wazi mlango wa mazungumzo na Moscow, akisema japokuwa "amevunjwa moyo" na Rais Vladimir Putin wa Russia, lakini "hajaishana naye."

Akizungumza na waandishi wa habari, Peskov ameyaelezea matamshi ya Trump kuwa ni "mazito sana."

"Bila shaka tunahitaji muda wa kuchambua kile kilichosemwa huko Washington. Na ikiwa Rais Putin atahisi ni muhimu na ni kwa wakati gani, bila shaka atatoa maoni yake" ameeleza msemaji huyo wa Kremlin.

Sambamba na hayo, Peskov amebainisha kuwa mabadiliko ya msimamo yaliyoonyeshwa hivi karibuni na Trump hayatatafsiriwa huko Kiev kama ni wito wa amani.

Amefafanua kwa kusema: "inavyoonekana, maamuzi kama hayo yanayofanywa Washington, katika nchi za NATO, na moja kwa moja kutoka Brussels, hayatafsiriwi na upande wa Ukraine ishara ya kuelekea kwenye amani, bali ni ishara ya kuendeleza vita".../