Kupinga Uturuki ombi la Marekani la kuacha kununua gesi ya Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i133436-kupinga_uturuki_ombi_la_marekani_la_kuacha_kununua_gesi_ya_russia
Uturuki imekataa ombi la Marekani la kuitaka Ankara isinunue gesi kutoka Russia na kusema kuwa, haiwezi kuacha kununua gesi ya Russia kwa sababu imesaini makubaliano ya gesi na nchi hiyo na itaendelea kuheshimu makubaliano hayo.
(last modified 2025-11-21T09:00:33+00:00 )
Nov 21, 2025 09:00 UTC
  • Kupinga Uturuki ombi la Marekani la kuacha kununua gesi ya Russia

Uturuki imekataa ombi la Marekani la kuitaka Ankara isinunue gesi kutoka Russia na kusema kuwa, haiwezi kuacha kununua gesi ya Russia kwa sababu imesaini makubaliano ya gesi na nchi hiyo na itaendelea kuheshimu makubaliano hayo.

Kituo cha Kupambana na Taarifa Potofu cha serikali ya Uturuki kimetangaza kwamba Ankara itaendelea kunua gesi kutoka Russia hata kama madola ya Magharibi yanadai kuwa nchi hiyo imetia saini mkataba wa kununua gesi kutoka Marekani hivyo inapaswa kuacha kunua gesi kutoka Russia. Uturuki inasema kuwa, mkataba wake na Russia ulitiwa saini zamani na manunuzi ya gesi ya Russia utaendelea kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Taarifa ya kituo hicho imesema: "Madai yaliyochapishwa katika baadhi ya vyombo vya habari kwamba Uturuki itaacha kununua gesi ya Russia kwa sababu Ankara imesaini makubaliano ya kununua gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) kutoka Marekani na kwa sababu hivyo, mgogoro wa nishati unakaribia nchini humo, ni taarifa za uongo zisizo na ukweli wowote."

Taarifa hiyo imesisitiza kwamba baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi vimedai kuwa Uturuki inakusudia kufunga mikataba ya kununua gesi kutoka nchi nyingine na kuachana na Russia.

Kituo cha Kupambana na Taarifa Potofu cha serikali ya Uturuki kimesema kwamba, Moscow inaendelea kupeleka gesi yake nchini Uturuki bila ya usumbufu wowote kwa mujibu wa mikataba ya muda mrefu iliyotiwa saini na nchi hizo mbili. Taarifa hiyo imesisitiza pia kwamba: "Kwa kuwa na mabomba imara ya gesi, miundombinu ya LNG na vituo vya kuhifadhia gesi, Uturuki ni moja ya nchi zinazoaminika sana katika eneo hilo kwenye suala zima la usalama wa usambazaji wa gesi, na hakuna hatari ya kuvurugika usambazaji wa gesi asilia au mgogoro wa nishati, iwe ni hivi sasa au katika majira yajayo ya baridi kali."

Njia ya bomba la gesi la TurkStream

 

Ni hivi karibuni tu ambapo Alexei Ivanov, Kaimu Balozi wa Russia nchini Uturuki alibainisha kuwa, mabomba yanayojulikana kwa majina ya "Mkondo wa Uturuki" na "Mkondo wa Bluu" yanaendelea kufanya kazi kwa kiwango cha juu, na gesi ya Russia inaendelea kupelekwa nchini Uturuki kupitia Bahari Nyeusi. Takwimu za miezi minane ya kwanza ya mwaka huu wa 2025 zinaonesha kuwa mauzo ya gesi ya Russia kwa Uturuki yameongezeka kwa karibu asilimia 20, licha ya vikwazo vya madola ya Magharibi dhidi ya Moscow. Alexander Frolov, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Nishati la Russia amesema kuwa ongezeko hilo linatokana na usalama wa miundombinu ya gesi ya Russia na uaminifu wake katika usambazaji wa nishati hiyo muhimu kwa Uturuki.

Uturuki imekuwa na nafasi muhimu katika masuala ya nishati kwenye eneo la Eurasia hasa katika miaka ya hivi karibuni. Kwa sababu Uturuki iko kwenye eneo maalumu la kijiografia na inajulikana kwa jina la njia kuu ya kusafirishia nishati ya gesi na mafuta. Kwa muktadha huo, uhusiano wa Uturuki na Russia katika masuala ya nishati ni muhimu sana. Licha ya mashinikizo makubwa ya madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani, Ankara hadi sasa imepinga kufuata siasa za Magharibi kwenye suala hilo na miongoni mwa sababu za kufanya hivyo ni kwamba: 

Mosi, Uturuki ni tegemezi sana kwa nishati ya gesi ya Russia. Uturuki huingiza sehemu kubwa ya mahitaji yake ya gesi asilia kutoka Russia. Miradi kama vile bomba la TurkStream, ambalo husafirisha gesi ya Russia kupitia Bahari Nyeusi hadi Uturuki na kisha Ulaya, inaonesha kina kikubwa cha utegemezi wa Ankara na nchi za Ulaya kwa gesi ya Russia. Uhakika wa mambo ni kuwa, haiwezekani kwa Uturuki kuacha kutumia gesi ya Russia, iwe ni kwa mtazamo wa kiuchumi au mtazamo wa kiutaalamu. Hakuna sehemu yoyote inayoweza kuziba kwa haraka pengo la gesi ya Russia inayoingia Uturuki na baadaye kwenye nchi za Ulaya. 

Pili, kuna mambo mengine muhimu sana ya kuzingatiwa hasa gharama za nishati yenyewe. Kuingiza Uturuki gesi kutoka Russia kwa kawaida hufanywa chini ya mikataba ya muda mrefu na kwa bei nafuu sana. Sasa kuvunjwa mikataba kama hiyo kutalemaza kila kitu nchini Uturuki na kupandisha vibaya bei za nishati na hivyo kuleta mashinikizo makubwa si kwa viwanda vya ndani ya Uturuki tu, bali pia kutasababisha malalamiko makubwa ya wananchi kutokana na kuzidi kupanda bei bidhaa na kufanya hali yao ya maisha kuwa nguvu zaidi.

Tatu ni kuhusiana na kwamba Rais Recep Tayyip Erdogan na serikali yake wanajaribu kuonesha kuwa siasa na maamuzi yao ni ya ndani ya Uturuki, si amri kutoka kwa madola kigeni. Serikali hiyo imejitangaza kwa wananchi kuwa inajali maslahi yao na maslahi ya taifa na ndio maana mara kwa mara inakuwa inapingana na sera za madola ya Magharibi. Suala la gesi na nishati ni suala la kitaifa, hivyo tunaweza hata kusema kwamba haiwezekani kwa Uturuki kufumbia macho maslahi yake ya kitaifa na kufuata siasa za kutwishwa za madola ya Magharibi kuhusu mikataba yake ya nishati na Russia.