Israel yaendelea kumwaga damu za Wapalestina, yaua 20 Gaza
Mashambulizi mapya ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel yamewaua shahidi watu wasiopungua 20, wakiwemo watoto wadogo katika Ukanda wa Gaza.
Mashuhuda wanasema vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni vimetumia droni na makombora, ambayo mbali na kusababisha maafa, lakini pia yamesababisha uharibifu mkubwa katika maeneo yaliyolengwa.
Hivi sasa, anga ya Gaza na Khan Younis, ikiwa ni pamoja na barabara kuu zinazoelekea katika kituo cha matibabu cha Nasser Medical Complex, imejaa ndege zisizo na rubani na ndege za kivita za Israel, na kufanya uchukuzi wa ardhini kuwa hatari zaidi.
Msemaji wa Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina (PRCS) amesema shirika hilo limearifiwa leo asubuhi kwamba, uhamishaji wa wagonjwa na waliojeruhiwa kupitia kivuko cha Rafah umesimamishwa.
Haya yanajiri siku chache baada ya Wapalestina wengine 31, wakiwemo watoto sita, kuuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Jiji la Gaza na mji wa Khan Younis katika Ukanda wa Gaza.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza imesema Wapalestina karibu 600 wameuliwa shahidi na jeshi la utawala wa Kizayuni tangu usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani huko Gaza ulipoanza kutekelezwa Oktoba 10, 2025.
Wakati huo huo, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ) imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kushiriki katika maandamano ya hasira na shughuli za mashinikizo dhidi ya mashambulizi na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.