Pompeo aanika nafasi ya US katika ghasia za karibuni nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136196-pompeo_aanika_nafasi_ya_us_katika_ghasia_za_karibuni_nchini_iran
Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA, Mike Pompeo, amekiri kwamba, Washington ilikuwa na mchango wa moja kwa moja katika ghasia za hivi karibuni nchini Iran, akisema Marekani "iliwasaidia moja kwa moja" wafanya fujo.
(last modified 2026-02-03T03:11:34+00:00 )
Feb 03, 2026 03:11 UTC
  • Pompeo aanika nafasi ya US katika ghasia za karibuni nchini Iran

Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA, Mike Pompeo, amekiri kwamba, Washington ilikuwa na mchango wa moja kwa moja katika ghasia za hivi karibuni nchini Iran, akisema Marekani "iliwasaidia moja kwa moja" wafanya fujo.

Katika mahojiano na Kanali ya 13 ya Israel jana Jumatatu, Pompeo amepinga mtazamo kwamba, Rais Donald Trump alifeli katika ahadi yake ya 'kuwapelekea msaada waandamanaji' nchini Iran. Amesisitiza kuwa, "Sidhani kama hivyo. Msaada ulikuja ... msaada mwingi. Huenda tusiuone wote ... Huenda tusijue yote, lakini Marekani inajaribu kuwasaidia."

Alipoulizwa kama Trump alipoteza fursa ya "kupindua" serikali ya Iran, Pompeo ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani hakukubaliana na wazo hilo pia.

Matamshi yake yamefichua kwamba, licha ya kauli za mara kwa mara za utawala wa Trump kuhusu kutafuta suluhisho la amani na Iran, lakini Washington nyuma ya pazia inafanya hima ili kufanya "mabadiliko ya utawala" nchini Iran.

Pompeo hapo awali alikuwa amefungamanisha ghasia zilizoshuhudia mwezi uliopita nchini Iran na mashirika ya ujasusi ya Marekani na Israel. Wakati wa ghasia hizo mnamo Januari 2, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa, "Heri ya Mwaka Mpya kwa kila Muirani mabarabarani. Pia kwa kila ajenti wa Mossad anayetembea kando yao."

Maandamano ya amani yalianza mwishoni mwa Desemba katika mitaa ya kibiashara ya Iran kufuatia kushuka kwa thamani ya sarafu ya rial ya Iran mkabala wa dola ya Marekani. Hata hivyo, kufikia mwanzoni mwa Januari, maandamano hayo yaligeuka na kuwa ghasia za vurugu baada ya magaidi na maajenti wa Israel na Marekani kuingia kwenye mikusanyiko ya waandamanaji, wakitumia risasi hai dhidi ya maafisa usalama na raia.

Mnamo Januari 12, mamilioni ya Wairani walishiriki katika maandamano ya kitaifa kuunga mkono Jamhuri ya Kiislamu, na baada ya hapo ghasia zilififia haraka, na hatimaye kuisha.