Jalali: Madai ya Trump kwamba anawaunga mkono Wairani hayana msingi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136256-jalali_madai_ya_trump_kwamba_anawaunga_mkono_wairani_hayana_msingi
Balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali amepuuzilia mbali matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani Donald Trump akidai kuwa analiunga mkono na kulisaidia taifa la Iran, akisisitiza kuwa madai hayo hayana msingi wowote.
(last modified 2026-02-04T10:55:16+00:00 )
Feb 04, 2026 10:55 UTC
  • Jalali: Madai ya Trump kwamba anawaunga mkono Wairani hayana msingi

Balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali amepuuzilia mbali matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani Donald Trump akidai kuwa analiunga mkono na kulisaidia taifa la Iran, akisisitiza kuwa madai hayo hayana msingi wowote.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika jana usiku, Jalali ameashiria historia ya zaidi ya miongo minne ya vikwazo vikali vya Washington dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba, "Mtu huyo (Trump) ambaye nchi yake imekuwa ikiliwekea vikwazo vikubwa taifa la Iran, na kusababisha ugumu wa kiuchumi na mateso kwa watu wetu, leo hii anadai kwa udanganyifu kuwa anatuunga mkono."

Itakumbukwa kuwa, mwezi uliopita wa Januari, Trump alihamasisha waziwazi vurugu kwa kuwataka waandamanaji wenye silaha kutwaa taasisi za serikali, na kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran iwapo magaidi hao wangedhuriwa.

Aliwataka wafanya fujo kuendeleza vuruga zao za umwagaji damu na uharibifu, akiwaambia "msaada upo njiani." Vurugu hizo ambazo zilichochewa na Marekani na utawala haramu wa Israel, zilisababisha uharibifu mkubwa wa mali za umma na binafsi,  taasisi za serikali, miundombinu ya huduma za umma, mbali na vifo vya maelfu ya raia na maafisa usalama.

Aidha Balozi wa Iran nchini Russia amegusia kuhusu kumbukumbu chungu wakati wa janga la Corona, ambapo Marekani si tu ilishadidisha vikwazo dhidi ya taifa hili, lakini pia iliweka vizingiti kwa nchi hii kupokea chanjo za virusi hivyo vilivyoua mamiloni ya watu duniani.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameeleza kuwa, "Hatujasahau kwamba wakati Iran ilipohitaji kupewa rasilimali zake za kifedha, dola bilioni saba zilizokuwa Korea Kusini ili kupambana na mripuko wa COVID-19, Marekani ilizuia kutolewa kwa fedha hizo zilizokusudiwa kutibu wagonjwa."