Mashambulizi ya droni yaua watu 15 Kadugli, kusini mwa Sudan
Raia wasiopungua 15, wakiwemo watoto saba, wameuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika mji wa Kadugli kusini mwa Sudan. Hayo yamesemwa na kundi la kujitolea la wenyeji na mashuhuda wa hujuma hiyo ambao wameeleza kuwa, mashambulizi hayo yamejiri saa chache baada ya jeshi la Sudan kutangaza kuvunja mzingiro wa miaka mingi dhidi ya mji wa Kadugli.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesema Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kimelenga vitongoji kadhaa vya makazi na Kituo cha Afya cha Al-Shartai katika mashambulizi hayo. Kundi hilo limelaani mashambulizi hayo na kuyaeleza kuwa "ukiukwaji mkubwa" wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
"Waathiriwa wengi walikuwa wagonjwa waliokuwa wakipokea matibabu ndani ya kituo hicho cha afya wakati wa hujuma," mmoja wa mashahuda huko Kadugli ameambia Xinhua, akiongeza kuwa shambulio hilo lilitokea saa kumi alasiri ya jana.
Mapema jana Jumanne, Jeshi la Sudan lilitangaza habari ya kuvunja mzingiro uliowekwa na waasi dhidi ya mji huo muhimu wa Kadugli. Hayo yalitangazwa na Rais wa mpito na Mkuu wa Jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.
Mji huo ambao ni makao makuu ya jimbo la Kordofan Kusini, na ambao Umoja wa Mataifa ulisema ulikumbwa na baa la njaa mwaka uliopita, umekuwa chini ya mzingiro kwa zaidi ya miaka miwili, tangu vita vya Sudan vilipooanza takriban miaka mitatu iliyopita kati ya jeshi na waasi wa RSF.
Mzingiro dhidi ya mji huo uliwekwa na wapiganaji wa RSF na washirika wao, kundi la Sudan People’s Liberation Movement-North linaloongozwa na Abdelaziz al-Hilu.
Mzingiro huo wa muda mrefu umelazimisha karibu asilimia 80 ya wakazi 183,750 wa Kadugli kukimbia makazi yao, kutokana na uhaba mkubwa wa chakula, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.