Kitengo cha "Kundi 26" cha RSF chajisalimisha kwa jeshi la Sudan
-
Wapiganaji wa RSF
Shirika la Habari la Sudan SUNA limetangaza kuwa, kitengo kimoja cha Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF kimejisalimisha kwa jeshi na kukabidhi wanajeshi wake na vifaa kamili vya kijeshi.
Kwa mujibu wa SUNA zoezi hilo lilifanyika siku ya Ijumaa.
Shirika hilo limesema, kikosi hicho ni sehemu ya "Kundi 26" la RSF, lakini halikutaja idadi ya wapiganaji waliohusika wala aina ya vifaa vilivyokabidhiwa.
SUNA imebainisha kuwa kundi hilo lilipokelewa na Al-Nour Ahmed Adam, anayejulikana kama Al-Nour al-Qubba, akiwa pamoja na maafisa wa ngazi ya juu kutoka jeshi la Sudan na Idara ya Intelijensia ya Taifa.
Al-Nour al-Qubba, mmoja wa waanzilishi wa RSF, alihamia upande wa jeshi rasmi mwezi Aprili, baada ya hapo awali kuhudumu kama kamanda wa ngazi ya juu katika vikosi hivyo vya usaidizi wa haraka na kushiriki katika mapigano ya kuuteka mji wa El Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini, mnamo mwezi Oktoba 2025.
Amesema, jeshi limelipokea rasmi kundi hilo lililojisalimisha na kwamba matukio kama hayo ya kujisalimisha yanaendelea, huku idadi ya wanachama wengi zaidi wa RSF wakijiunga na jeshi katika miezi ya hivi karibuni.
Al-Nour al-Qubba ameielezea RSF kama kundi lisilo na "misingi, lengo wala mkakati," akiongeza kuwa uungaji mkono wa kigeni kwa kundi hilo "hautabadilisha matokeo ya vita" na unalenga "maslahi binafsi tu."
Othman Al-Nour Hasab Khalil, mmoja wa wapiganaji waliojisalimisha, amewasihi wenzake wa zamani katika RSF kuacha mapigano na kujiunga na jeshi rasmi.
Tangu mwezi wa Aprili 2023, Sudan imekumbwa na vita vya ndani kati ya jeshi na RSF; mzozo ambao umesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu, kuwafanya mamilioni ya wengine kulazimika kuyahama makazi yao, na kuchochea moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani…/