Seneta wa Nigeria: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, nembo ya uhuru duniani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136254-seneta_wa_nigeria_mapinduzi_ya_kiislamu_ya_iran_nembo_ya_uhuru_duniani
Seneta Shehu Sani wa Nigeria ambaye pia ni mkuu wa Jukwaa la Haki za Kiraia la Nigeria (CRCN), amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979 ni vuguvugu la mwamko wa kihistoria dhidi ya dhulma na ubeberu wa maajinabi, akiyaelezea mapinduzi hayo kama kigezo cha mataifa yanayokandamizwa duniani kote.
(last modified 2026-02-05T02:33:18+00:00 )
Feb 04, 2026 10:24 UTC
  • Seneta wa Nigeria: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, nembo ya uhuru duniani

Seneta Shehu Sani wa Nigeria ambaye pia ni mkuu wa Jukwaa la Haki za Kiraia la Nigeria (CRCN), amesema Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ya mwaka 1979 ni vuguvugu la mwamko wa kihistoria dhidi ya dhulma na ubeberu wa maajinabi, akiyaelezea mapinduzi hayo kama kigezo cha mataifa yanayokandamizwa duniani kote.

Katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press kwa mnasaba wa maadhimisho ya miaka 47 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Seneta Sani amesema Mapinduzi ya Kiislamu yalienda mbali zaidi ya kuwa tukio la kitaifa.

Mtunga sheria huyo wa Nigeria amebainisha kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu yanaonyesha kwamba nchi ambazo zinaonekana dhaifu zinaweza kukabiliana na tawala za kiimla, kudumisha uhuru, na kuchangamkia fursa za ustawi hata zikiwa chini ya vikwazo na mashinikizo ya nje.

Seneta Sani ameyaelezea Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kama "nembo ya kimataifa ya uhuru," akisisitiza kwamba ingawaje mapinduzi mengine yametokea katika pembe tofauti za dunia, lakini hakuna ambayo yamekuwa na athari duniani kote kama ya Iran.

Amesema: Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka wa 1979 ni moja ya matukio makubwa ya kihistoria ambapo watu walipinga udhalimu, udikteta, utawala wa kigeni, na ukoloni. Ni mapinduzi ambayo yataendelea kukumbukwa kwa vizazi vingi.

Kadhalika Seneta huyo wa Nigeria ameeleza bayana kuwa, "Kabla ya (mapinduzi) haya, kulikuweko na mapinduzi ya Cuba, Urusi, na Marekani, miongoni mwa mengine, lakini hakuna yaliyougusa ulimwengu na kuwa nembo ya ustahimilivu na uhuru kama Mapinduzi ya Iran."

Akiashiria mafanikio ya Iran licha ya vikwazo vya Wamagharibi, mbunge huyo wa Baraza la Seneti la Nigeria amesema: "Tafakari iwapo Iran ingeliachiwa kikamilifu kujiendeleza; maendeleo yake yangeweza kuwa makubwa zaidi. Hata hivyo, licha ya vikwazo, Iran imepiga hatua kubwa katika nyuga za sayansi, teknolojia, kilimo, na viwanda."