Marais wa Iran na Marekani watia saini kidijitali Makubaliano ya kumaliza vita
-
Rais Pezeshkian
Hati ya makubaliano (MoU) kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani sasa imetiwa saini rasmi na marais wa nchi hizo mbili baada ya maandishi yake kukamilishwa, na hivyo makubaliano hayo kuanza kutekelezwa. Hayo yametangazwa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Jumatano usiku.
Esmaeil Baghaei ameliambia Shirika la Utangazaji la Iran (IRIB) kwamba ilikubaliwa kuwa hati ya makubaliano kati ya Iran na Marekani itatiwa saini kwa njia ya kidijitali na Marais Masoud Pezeshkian wa Iran na Donald Trump wa Marekani, na ameongeza kuwa hakutakuwa na hafla ya kutia saini nchini Uswisi.
Msemaji huyo amefafanua kwamba uamuzi wa kufanya makubaliano hayo, yajulikanayo kama Mapatano ya Islamabad, yatiwe saini na viongozi wa juu kabisa wa nchi zote mbili ulifanywa kwa makusudi kutokana na uzoefu wa nyuma.
Baghaei amebaini kuwa wakati maandishi yanatiwa saini na marais wa nchi zote mbili, kuvunja makubaliano hayo kutakuwa na gharama kubwa zaidi. Ameongeza kuwa: "Kwa kuzingatia uzoefu wetu wa zamani, tulipendelea iwe hivyo."
Baghaei ameonya kuwa utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha vita na Marekani utakuwa mgumu zaidi kuliko kuyatia saini, akisisitiza kuwa Tehran haijasahau mafunzo ya vita na itafuatilia kwa makini utekelezaji wa wajibu wa Marekani.
Amesema kuwa taasisi za diplomasia za Iran, kwa kuungwa mkono kikamilifu na wananchi, zimefanikisha makubaliano yanayolinda maslahi ya taifa.
Msemaji huyo amesisitiza pia kuwa Iran haitasita kujibu iwapo Marekani haitatekeleza wajibu wake uliokubaliwa.
Baghaei ameongeza kuwa uamuzi wa Iran wa kuahirisha mazungumzo ya nyuklia hadi hatua inayofuata ulikuwa wa busara, huku kipaumbele kikiwekwa kwanza katika kumaliza vita. Amefafanua kuwa: “Kuanzia wakati MoU inapoanza kutekelezwa , tutakuwa na siku 60 za kujadiliana kuhusu suala la nyuklia na kuondolewa kwa vikwazo. Ikiwa mazungumzo yatafikia hitimisho mapema zaidi, itakuwa bora. Lakini kutokana na ugumu wa suala hilo, muda wa siku 60 ni wa msingi, na iwapo itahitajika unaweza kuongezwa.”
Ameongeza kuwa makubaliano hayo yanaeleza wazi kwamba mazungumzo yajayo yatahusisha tu suala la nyuklia na kuondolewa kwa vikwazo.
Baghaei amesisitiza kwamba Iran haijawahi kuwaacha washirika wake, akisema kusitishwa kwa mapigano nchini Lebanon ni jambo muhimu kwa Iran kama ilivyo kumalizika kwa vita dhidi ya Iran yenyewe.
Amethibitisha pia kuwa kuondolewa kwa vikwazo vya mafuta tayari kumeanza, akieleza kuwa sambamba na MoU hiyo, Tehran ilifanya mazungumzo ya ziada kuhusu kuachiliwa kwa mali zilizogandishwa, ujenzi upya wa uharibifu uliosababishwa na vita, pamoja na kuondolewa kwa vikwazo vya mafuta.
Msemaji huyo pia alithibitisha kuwa Iran iko katika hatua za mwisho za kuanzisha mfumo mpya wa usimamizi wa Lango-Bahari la Hormuz, kwa kushirikiana na Oman.
Baghaei pia amesema Iran itaendelea kurekodi na kufuatilia kisheria uhalifu uliofanywa dhidi ya wananchi wake wakati wa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vilivyoanza Februari 28.
Aidha amesisitiza kuwa hadhi ya Iran kama dola yenye nguvu kubwa si jambo la nadharia. Amesema: “Tumezishinda tawala mbili zenye silaha za nyuklia, pamoja na nchi nyingine zilizowaunga mkono."
Makubaliano ya MoU kati ya Iran na Marekani yalikamilishwa Jumapili baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo makali yaliyosimamiwa na Pakistan, kwa msaada wa baadhi ya nchi nyingine za kanda.
Hati hiyo ya MoU yenye nukta 14 inaweka bayana ahadi za haraka kwa upande wa Marekani na kibaraka wake Mzayuni, za kusitisha uchokozi wa kijeshi katika pande zote, ikiwemo Lebanon, huku ikisisitiza kuheshimu mamlaka ya Iran, ukamilifu wa ardhi yake, na kutoingilia mambo ya ndani ya Iran.
Aidha, inaweka ratiba ya mazungumzo ya kina ambayo yanatarajiwa kuzaa makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60. Mbali na vipengele vya kiusalama, hati hiyo inashughulikia usalama wa baharini, dhamana za usafirishaji wa kibiashara, kuondolewa kwa vikwazo, misaada ya ujenzi wa uchumi, na kufunguliwa hatua kwa hatua kwa mali za Iran zilizokuwa zimezuiwa nje ya nchi.
Pia, inajumuisha vipengele vinavyohusiana na uhakikisho wa nyuklia, mifumo ya ukaguzi chini ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), na kudumisha hali ya sasa ya muda (status quo) wakati wa mazungumzo. Mfumo madhubuti wa utekelezaji na ufuatiliaji pia umeainishwa katika hati hiyo.
Hatimaye, makubaliano hayo yanalenga kupata idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hatua inayoashiria nia ya kuyaimarisha makubaliano yoyote ya mwisho ndani ya mfumo wa kisheria wa kimataifa.
Hati hiyo ya maelewano imekuja kufuatia mhimili wa Marekani na Israel kukumbwa na kipigo cha fedheha katika uwanja wa vita, hali iliyowashurutisha kulegeza misimamo mbele ya Iran wakati wa mazungumzo hayo.