Je, vita vya Iran vilisambaratisha vipi ngano ya nguvu isiyoshindwa ya Marekani?
"Vita na Iran vimefichua ukweli mchungu kwa Marekani; Trump alifanya makosa makubwa na hatari kwa kuanzisha vita hivi na hatimaye kutoka kwenye vita akiwa dhaifu kijeshi, kidiplomasia na kiuchumi."
Haya ni maneno ya bodi ya wahariri ya gazeti la New York Times ambayo yanaonyesha uwepo wa pengo kubwa katika tathmini ya wasomi wa Marekani kuhusu makosa ya mahesabu ya kimkakati yaliyoisababishia Washington gharama kubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Utawala wa Donald Trump ulianzisha vita kwa kuweka malengo kadhaa makuu na ya wazi: "Kujisalimisha Iran bila masharti," "kubadilishwa mfumo unaotawala," "kusimamishwa kikamilifu urutubishaji," na "kuondolewa nchini Iran mada zote za nyuklia." Lakini kama gazeti la New York Times linavyosisitiza, kumalizika kwa vita sio tu hakukutimia kwa kufikiwa hata lengo moja kati ya malengo hayo, bali pia kumeiacha Marekani katika hali ya kufedhehesha na kuilazimu itie saini makubaliano ambayo miezi miwili iliyopita yalionekana kama ishara ya kushindwa.
Hii si mara ya kwanza kwa tamaa za kijeshi za Marekani kukabiliwa na hali halisi ya kijiopoliti katika eneo la Asia Magharibi. Uzoefu wa Afghanistan, Iraq, na hata uingiliaji mdogo zaidi wa kijeshi wa Marekani katika eneo umeonyesha wazi kuwa ubora wa kijeshi hauambatani daima na ushindi wa kisiasa. Taasisi ya kifikra ya Marekani Rand, imeonya mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni kwamba mzozo wowote wa moja kwa moja na Iran hautakuwa na suluhisho la wazi, kwa kutilia maanani uwezo mkubwa wa Tehran katika nyanja mbalimbali, kuenea kwa ukubwa wa kijiografia wa mgogoro, na kuathirika kimataifa kwa miundombinu ya nishati. Moja ya mada muhimu zaidi za ripoti ya New York Times ni kushindwa kwa dhana ya "kusambaratika haraka kwa mfumo wa utawala wa Iran". Dhana ambayo Benjamin Netanyahu wa Israel alimtwisha Trump wa Marekani. Wataalamu wengi wa Marekani, akiwemo Stephen Walt, mhadhiri mashuhuri wa mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Harvard, wamesisitiza kwa miaka mingi kwamba mashinikizo ya nje na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran kwa kawaida huwa na matokeo kinyume, ambapo badala ya kudhoofisha mshikamano wa ndani, huimarisha hisia za utaifa nchini.
Licha ya kupata hasara kubwa za kibinadamu na miundombinu, Iran iliweza kujenga upya haraka muundo wake wa kuchukua maamuzi na uwezo wa kioperesheni ambapo ilifanikiwa kugeuka kuwa mchezaji ambaye aliulazimisha upande wa pili kukiri kwa fedheha uzito wake wa kimkakati. Hili limewafanya baadhi ya wachambuzi wa nchi za Magharibi kuzungumzia "ushindi wa kimkakati wa Iran," suala ambalo halimaanishi ushindi kamili tu, bali pia ni kushindwa kwa upande wa pili kufikia malengo uliyoyatangaza.
Matokeo mengine ya vita hivi ni taathira zake kwa itibari ya kimataifa ya Marekani. Baraza la wahariri la New York Times linasema kwamba Washington sasa inaonekana kuwa dhaifu kuliko huko nyuma machoni pa waangalizi wengi wa kimataifa. Jarida la Foreign Policy pia limeonya katika changanuzi zake kwamba mapungufu makubwa katika maghala ya silaha ya Marekani katika vita virefu yanaweza kupunguza nguvu ya uzuiaji wa hujuma wa nchi hiyo dhidi ya wapinzani wake kama China.
Kwa mtazamo wa kiuchumi, vita hivi pia vimethibitisha kuwa Lango-Bahari la Hormuz linasalia kuwa moja ya malango muhimu zaidi katika uchumi wa dunia. Kile kilichotajwa na Trump mwishoni mwa vita kuwa "kufunguliwa Lango-Bahari la Hormuz" kwa kweli ni kurejea katika hali ile ile iliyokuwepo kabla ya kuanza vita. Tofauti kuu ikiwa kwamba mara hii masoko ya kimataifa yametambua kuwa Iran ina zana nyingi madhubuti za kuathiri mtiririko wa nishati duniani ikiwa itahisi kuwa uhai wake unakabiliwa na tishio la kuwepo au kutokuwepo. Utambuzi huu pekee unatosha kuongeza gharama za kimkakati za mapambano yoyote ya baadaye.
Jambo jingine muhimu ni mgogoro wa uhalali wa kufanya maamuzi ndani ya Marekani. Gazeti la New York Times linazungumzia waziwazi kuhusu ukiukaji wa Trump wa Katiba ya Marekani na kuipuuza Congress katika maamuzi ya vita. Suala hili limeibua pengo la muda mrefu lililopo kuhusu mamlaka ya rais na jukumu la Congress katika kutangaza vita na hivyo kuibua tena nchini mjadala wa kisiasa kuhusu jambo hilo. Kupitishwa kwa miswada ya kupunguza nguvu za vita za rais katika Congress pia ni ishara ya wasiwasi huu unaokua.
Hatimaye, moja ya masomo muhimu zaidi yaliyopatika katika vita vya karibuni ni kushindwa kwa "dhana potofu ya kubuniwa mfumo wa kikanda kupitia nguvu za kijeshi." Marekani kwa mara nyingine tena umejifunza kwamba nguvu ya kijeshi, hata iwe haribifu kwa kiwango gani, lakini si dharura kwamba siku zote itakuwa na uwezo wa kuwa na matokeo yanayohitajika kisiasa. Ikiwa majigambo ya kijeshi yataandamana na uelewa pungufu wa jamii inayolengwa pamoja na utata wa eneo, yanaweza kugeuka ghafla kuwa madhara makubwa kwa mchokozi.
Ripoti ya New York Times kwa kweli kabla ya kuwa simulizi ya kushindwa rais wa nchi, ni tahadhari kuhusu kudhoofika kwa mojawapo ya mbinu muhimu za kisiasa za Marekani. Mbinu inayodhaniwa kimakosa kuwa inaweza kutumika katika ulipuaji mabomu, matumizu ya vikwazo na vitisho kwa ajili ya kubadilisha hali halisi ya kijiopolitiki ya eneo linalolengwa. Vita vya Iran vimethibitisha kwamba zama za utatuzi rahisi wa migogoro tata kupitia mbinu za kijeshi na vitisho zimepitwa na wakati, na upuuzaji wowote wa ukweli huu bila shaka utakuwa na gharama kubwa, si kwa Washington tu, bali kwa mfumo mzima wa dunia.