Mamia waandamana Brussels wakitaka kuwekewa vikwazo Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i139252-mamia_waandamana_brussels_wakitaka_kuwekewa_vikwazo_israel
Mamia ya watu walifanya maandamano jana Alhamisi Brussels, Ubelgiji kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya.
(last modified 2026-06-19T03:46:24+00:00 )
Jun 19, 2026 03:44 UTC
  • Mamia waandamana Brussels wakitaka kuwekewa vikwazo Israel

Mamia ya watu walifanya maandamano jana Alhamisi Brussels, Ubelgiji kabla ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya.

Waandamanaji hao walitoa wito wa kuwekewa vikwazo Israel na kupigwa marufuku bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Maandamano hayo yalifanyika karibu na taasisi za Umoja wa Ulaya na yakiwashirikisha wanaharakati wa masuala ya kijamii, haki za binadamu na wanachama wa msafara wa kimataifa wa Flotilla ulioelekea Gaza hivi karibuni kupeleka misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wanaozingirwa na Israel katika eneo hilo.

Waandamanaji hao dhidi ya Israel walisisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unapasa kutumia ushawishi wake wa kiuchumi kuzidisha mashinikizo dhidi ya utawala wa Israel huku kukiwa na mvutano unaohusishwa na vita vya Gaza na upanuzi wa makazi ya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Maandamano hayo yaliitishwa na Kundi la kutetea haki za binadamu la Avaaz na kumjumuisha mwanaharakati wa masuala ya hali ya hewa wa Uswidi, Greta Thunberg.

Waandamanaji huko Brussels walibeba mabango yenye maandishi "EU, acheni kununua kile kinachoiba na Israel" na wametoa wito wa kuwekewa vikwazo bidhaa kama tende, parachichi na bidhaa zingine za kilimo zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.