Shirika la Anga za Juu la Iran kuzindua satalaiti ya Pars-2
-
Sateaiti iliyotengenezwa nchini Iran ya iitwayo Noor 3, ikirushwa katika anga za mbali 27 Septemba 2023.
Shirika la Masuala ya Anga za Juu la Iran linasonga mbele kwa kasi mpya, huku Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano akitangaza mipango ya uzinduzi ujao wa satalaiti ya "Pars 2" na kupelekwa angani Shahid Soleimani Satellite Constellation ifikapo mwisho wa mwaka huu.
Akizungumza Jumatano katika mkutano na wataalamu na mameneja wa Taasisi ya Utafiti wa Anga za Juu ya Iran, akiwemo Hassan Salarieh, mkuu wa Shirika la Anga za Juu la Iran (ISA), Sattar Hashemi amesifu mafanikio ya sekta ya anga za juu chini ya utawala wa sasa, akisisitiza kuwa maendeleo yaliyopatikana yametokana na juhudi za wasomi na wataalamu katika uwanja huo.
"Mtazamo wa Wizara ya Mawasiliano na Serikali ya Awamu ya 14 kuhusu tasnia ya anga za juu ni wa kimkakati, na uwanja huu una uwezo mkubwa wa kukuza kilimo bora, usimamizi wa rasilimali za maji na ardhi, na kuboresha utawala unaoendeshwa na data nchini," Hashemi amesisitiza.
Waziri Sattar Hashemi pia ameangazia uimara wa miundombinu ya anga za juu ya Iran katika kipindi cha vita, akielezea shughuli zinazoendelea kuwa ni mafanikio makubwa.
Akizungumzia miradi inayoendelea kutekelezwa, ameongeza kwamba "mipango muhimu inaendelea ili kuweka satalaiti ya 'Pars 2' kwenye obiti."
Pars-2 ni satalaiti ya kisasa, iliyotengenezwa ndani ya nchi, yenye usahihi wa hali ya juu ya kupiga picha, iliyotengenezwa na ISA ikiwa na dhamira kuu ya uchunguzi wa dunia, utambuzi wa mbali, na ufuatiliaji wa mazingira.
Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa Iran amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano wa kimataifa na kiteknolojia wakati jitihada za kujenga upya na kurekebisha sekta hiyo zikiendelea baada ya changamoto zilizosababishwa na vita vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.