Jihad Islami yailaumu Marekani kwa ukatili unaoendelezwa na Israel huko Gaza
Harakati ya Jihadi Islami ya Palestina imesema utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani lazima uwajibishwe kwa ukatili na vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na askari wa utawala vamizi wa Israel dhidi ya Wapalestina wa kawaida katika Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita.
Harakati hiyo imesema katika taarifa yake kwamba Washington inawajibika moja kwa moja kwa uhalifu unaoendelea Gaza, kwani inawalinda wahalifu wa kivita wa utawala wa Kizayuni dhidi ya kushtakiwa, na inawahimiza kukiuka sheria, kanuni za kibinadamu na kanuni za kimataifa.
"Shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya raia wa Palestina kwenye ufuo wa Khan Younis, ambalo limeua shahidi na kujeruhi baadhi ya watu, pamoja na kulipua nyumba na maeneo ya makazi, linaonyesha mbinu ya baraza la mawaziri la Israel, na uamuzi wake wa kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu bila kujali lolote," imesema taarifa hiyo.
Harakati hiyo imesisitiza kwamba utawala wa Tel Aviv, unataka kulazimisha hali mpya za kijeshi na kiusalama katika Ukanda wa Gaza, na kuzuia utekelezaji wa vifungu vya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Vyanzo vya matibabu vya Palestina vinasema shambulio la ndege zisizo na rubani za Israel limeua raia wawili wa Palestina waliokuwa wakielekea ufukweni na kuwajeruhi wengine kadhaa kusini mwa Gaza, siku ya Jumatano, ikiwa ni ukiukaji wa hivi karibuni wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa Oktoba 10 mwaka jana.
Vyanzo hivyo vimeliambia shirika rasmi la habari la Palestina, WAFA kwamba miili ya waathiriwa wawili na watu wanane waliojeruhiwa imepelekwa katika Hospitali ya Nasser.
Ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano uunaofanywa na Israel umeua Wapalestina wasiopungua 1,007 na kuwajeruhi wengine 3,165 tangu makubaliano yalipoanza kutekelezwa.