Nigeria: Mamia ya wanawake na watoto waliotekwa nyara na magaidi waachiliwa
-
Jeshi la Nigeria lawakomboa mateka
Mamia ya wanawake na watoto waliokuwa wametekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram kaskazini mashariki mwa Nigeria wameachiwa huru mwishoni mwa wiki.
Haikufahamika mara moja ni vipi matake walivyoachiliwa, ingawa jeshi limesema limetekeleza “operesheni ya uokoaji iliyotegemea taarifa za kijasusi”.
Utekaji nyara , mara nyingi kwa lengo la kudai kikombolea, umekuwa mbinu kuu ya magaidi wa Boko Haram katika uasi wao wa takribani miaka 17 dhidi ya serikali ya Nigeria, ambao umejikita zaidi katika maeneo ya kaskazini‑mashariki.
Samaila Kaigama, rais wa Jumuiya ya Vijana wa Borno Kusini (BOSYA), amesema kundi lake “limefanikisha kuachiliwa kwa wanawake na watoto wote 416 waliotekwa kutoka Ngoshe”.
Amesema mateka hao waliachiliwa siku ya Jumamosi.
Mohammed Ali Ndume, seneta kutoka jimbo la Borno, pia alithibitisha kuachiliwa kwao alipoongea na waandishi wa habari.
Kwa upande mwingine, jeshi la Nigeria limesema limetekeleza “operesheni ya uokoaji iliyoongozwa na taarifa za kijasusi” iliyowezesha kuachiliwa kwa watu 360.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, wanajeshi walikusanya taarifa za kijasusi na kutumia kile walichokiita “operesheni za kisaikolojia” ili kueneza hali ya kutokuaminiana ndani ya safu za waasi kabla ya “kuanza kwa awamu ya mashambulizi”.
Inasemekana magaidi hao walikuwa wanadai kikomboleo chaa mamilioni ya naira ili kuwaachilia mateka waliotekwa Ngoshe.
Makundi mbalimbali yenye silaha nchini Nigeria , yakiwemo ya magaidi wakufurishaji, magenge ya uhalifu, pamoja na makundi ya kujitenga, yamesababisha mgogoro mkubwa wa utekaji nyara kote Nigeria. Kulingana na ripoti ya SBM Intelligence, kampuni ya uchambuzi yenye makao Lagos, takribani dola milioni 1.66 zilikusanywa kama kikombolea kati ya Julai 2024 na Juni 2025.
Kijiji cha Ngoshe kiko chini ya kilomita 10 kutoka mpaka wa Cameroon katika milima ya Gwoza , eneo linalochukuliwa kuwa ngome ya Boko Haram, na kimekuwa kikishambuliwa mara kwa mara.
Tangu uasi wa Boko Haram ulipoanza mwaka 2009, ghasia za magaidi hao wakufurishaji nchini Nigeria zimezaa makundi kadhaa yenye silaha, na zimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu pamoja na kuwafanya mamilioni kuhama makazi yao. Kundi la Boko Haram hushirikiana na makundi ya kigaidi ya kimataifa kama vile Al Qaeda na ISIS au Daesh, ambayo inaaminika yalianzisha na mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi hasa Marekani.