Watu wenye silaha waua raia wasiopungua 30 jimboni Kaduna, Nigeria
Watu wasiopungua 30 wameuawa wakati watu wenye silaha waliposhambulia kijiji katika jimbo la Kaduna kaskazini magharibi mwa Nigeria. Hayo yamethibitishwa na wakazi wawili wa kijiji hicho.
Dogon Rana, katibu wa mkuu wa kijiji, amesema watu wenye silaha walivamia kijiji hicho mapema jana wakifyatua risasi bila mpangilio na kuchoma moto nyumba za wanakijiji. Watoto wanane walikuwa miongoni mwa waliouawa, huku watu wengine wanne wakipata majeraha.
Vitendo vya ukatili na machafuko vinavyofanywa na magenge yenye silaha na makundi mengine ya wahalifu vimekuwa ni changamoto kubwa ya usalama katika sehemu za kaskazini-magharibi na kaskazini-kati mwa Nigeria, ambapo jamii za maeneo hayo huwa mara nyingi walengwa wa mashambulizi ya mauaji.
Eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria linapambana na uasi wa hujuma za mauaji unaofanywa na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram na lile lililojitenga kutoka kundi hilo liitwalo ISWAP. Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo katika jimbo la Kaduna.
Kiongozi wa vijana Ishaya Dawa, ambaye ni mkazi mwingine wa kijiji kilichoshambuliwa, amesema washambuliaji hao walivamia kijiji cha Naridon katika eneo la serikali ya mtaa ya Kauru muda wa karibu na usiku wa manane na kuwafyatulia risasi wanakijiji.
Dawa amebainisha kuwa, baadhi ya wakazi waliuawa kwa kuchinjwa, akiongeza kuwa miili kadhaa ilikuwa imepelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
"Waathiriwa ni wanawake, watoto na wazee," ameeleza mkazi huyo na kuongeza kwamba, washambuliaji hao walichoma moto nyumba kabla ya kukimbia.
Kwa mujibu wa Ishaya Dawa alisema maafisa wa usalama walifika kijijini hapo asubuhi, saa kadhaa baada ya shambulio hilo…/