Raia zaidi ya 300 waliotekwa nyara Nigeria waokolewa katika operesheni kubwa
-
Raia zaidi ya 300 waokolewa kutoka kwa makundi yenye silaha
Nigeria imesema kuwa zaidi ya watu 300 waliotekwa nyara katika mashambulizi tofauti ya watu wenye silaha wameokolewa kupitia operesheni ya pamoja ya kiintelijensia na kiusalama.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano, ofisi ya Rais wa nchi hiyo imebainisha kuwa watu 163 kati ya hao waliokolewa walitekwa nyara mwezi Februari mwaka huu katika kijiji cha Woro katika Jimbo la Kwara na wengine 145 walitekwa nyara katika jimbo la Niger kaskazini-kati nchini Nigeria.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, raia hao waliokolewa kutoka katika eneo moja ndani ya msitu wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Kainji; na hadi sasa bado haijafahamika iwapo kuna washukiwa wowote waliotiwa nguvuni wakati wa oparesheni hiyo ya siku moja jana Jumatano.
Taarifa ya ofisi ya Rais wa Nigeria imeongeza kuwa, oparesheni ya jana ilitekelezwa na Kituo cha Taifa cha Kupambana na Ugaidi kwa kushirikiana na jeshi la ulinzi la nchi hiyo, jeshi la polisi na Idara ya Huduma za Serikali.
Watu waliookolewa wanaendelea kupata matibabu katika kambi ya kijeshi kabla ya kuunganishwa tena na familia zao.
Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria amepongeza kupatikana raia hao 300 na kuitaja operesheni hiyo kama ishara ya kuimarika kwa uratibu na mikakati miongoni mwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo.
Vitendo vya utekaji nyara kwa ajili ya kudai fidia vinavyofanywa na makundi ya uhalifu, wanagambo wenye uhusiano na kundi la kigaidi la Boko Haram na magenge mengine ya uhalifu ni tatizo kubwa nchini Nigeria, hasa katika maeneo ambayo hali ya usalama ni ya kiwango cha chini.