Iran yaishukuru China kwa uungaji mkono wake katika vita vya US,Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza hatua ya China ya kulaani vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Israel na Marekani dhidi ya ardhi na mamlaka ya kujitawala Iran, huku akisisitiza utayarifu wa Tehran wa kuimarisha zaidi uhusiano huo wa kirafiki na Beijing.
Katika mkutano na mwenzake wa China pambizoni mwa Mkutano wa 25 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) nchini China leo Jumatano, Abbas Araghchi ameishukuru Beijing kwa msimamo wake wa "kanuni, kujenga na ushawishi" katika majukwaa ya kimataifa, haswa katika mikutano ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kulaani hujuma na mashambulizi dhidi ya Iran.
Amemueleza waziri mwenzake wa China kuhusu matukio ya hivi karibuni kufuatia hujuma hizo na kusitishwa kwa mapigano hayo, akisisitiza kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na serikali zote duniani zina wajibu wa kudumisha amani na usalama katika eneo la Asia Magharibi na dunia kwa ujumla.
Sayyid Araghchi pia amesisitiza dhamira ya dhati ya serikali ya Iran ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kidugu, na ushirikiano wa kimkakati unaozingatia kuheshimiana na kuaminiana.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mkutano kikao cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai nchini China kwamba, utawala ghasibu wa Israel na Marekani zilifanya jinai za kivita dhidi ya Iran. Ameyataja mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel na Marekani dhidi ya Iran kuwa ni uhalifu wa kivita na ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na akataka jamii ya kimataifa itoe radiamali kali.
Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China kwa upande wake, amepongeza mbinu ya kuwajibika na ya kimantiki ya Iran katika kuzuia kushadidi mivutano na migogoro katika eneo la Asia Magharibi.