Jeshi la Wanamaji la Iran kuzindia zana mpya za kivita
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133668-jeshi_la_wanamaji_la_iran_kuzindia_zana_mpya_za_kivita
Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran, ametangaza mipango ya kuzindua vifaa vipya na kuunganisha meli mpya katika jeshi hilo.
(last modified 2025-11-28T03:11:33+00:00 )
Nov 28, 2025 02:46 UTC
  • Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran
    Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran

Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran, ametangaza mipango ya kuzindua vifaa vipya na kuunganisha meli mpya katika jeshi hilo.

Katika mkutano na waandishi wa habari kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Wanamaji la Iran, amesema kuwa kwa baraka za siku hii, kunazinduliwa zana mpya za Jeshi la Wanamaji. Amesema hatua hii inalenga kuwezesha jeshi hilo kushiriki kwa dhati zaidi katika maeneo ya bahari kuu na kuhakikisha usalama wa kiuchumi na njia za usafirishaji majini.

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Iran, akijibu kurejea kwa vikwazo na va madola ya magharibi dhidi ya Iran amesisitiza kuwa hatua hizo zimeleta matokeo kinyume, kwani meli za Iran zenye bendera ya taifa zinaendelea na safari katika bandari za dunia.

Amekumbusha kuhusu operesheni ya kihistoria ya  Kikosi Cha 86 cha Jeshi la Wanamaji la Iran  katika Bahari ya Pasifiki na kuitaja kuwa ishara ya kutokuwa na athari kwa vikwazo, hususan licha ya marufuku rasmi ya kupita katika Mfereji wa Panama.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2023  Marekani ilishindwa kuzuia kundi la 86 la manowari za Jeshi la Wanamaji la Iran kupita kwenye Mfereji wa Panama.

Kamanda Shahram Irani pia amegusia nafasi ya Iran katika kuhakikisha usalama wa bahari katika mwambao wa Bahari ya Hindi na kuongeza kuwa, '"Hadi sasa zaidi ya Misafara 103 ya Jeshi la Wanamaji la Iran imeshatumwa katika maji ya bahari kuu." Aidha amebaini kuwa,  hivi sasa vikosi viwili vipo katika majukumu ya kimataifa mashariki na kusini mwa bara la Afrika, na vikosi viwili vingine vinaendelea kujiandaa kwa safari. Admeri Shahram Irani amesisitiza kuwa uwepo huu wa kudumu ni sehemu ya utekelezaji wa sera za kijeshi za Iran za kuhakikisha usalama katika bahari kuu.