Kuondoka vikosi vya kigeni, suluhisho pekee la mgogoro wa Yemen
Kiongozi mmoja mwandamizi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa, kuendelea kuwepo wanajeshi vamizi ndani ya ardhi ya Yemen ni tatizo kuu la mgogoro wa nchi hiyo akisisitiza kwamba upatanishi wowote kutoka nchi jirani hausaidii, kwani wao wenyewe hao wapatanishi ndio wahusika wakuu wa mgogoro wa Yemen.
Abdul Malik al-Ejri amesema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuandika kwamba mapigano ya hivi karibuni ya silaha kati ya mamluki wa Saudi Arabia na Imarati katika maeneo ya kusini na mashariki mwa Yemen ni uthibitisho kwamba vikosi vya kigeni ndivyo vinavyochochea na kushadidisha mgogoro wa Yemen.
Aidha amepuuza madai ya Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) ya kudai kwamba umejiondoa kijeshi nchini Yemen na kusema kuwa, kudai kwa maneno tu hakutoshi na ametoa mwito wa kuondoka kikamilifu vikosi vyote vya kigeni vilivyobakia nchini Yemen.
Al-Ejri, ambaye pia ni mjumbe wa timu ya mazungumzo ya Yemen kwa upande wa Ansarullah, amesisitiza kwamba, hakuna nchi jirani inayoweza kuongoza suluhisho au upatanishi maadamu nchi hiyo inahusika moja kwa moja katika uchokozi dhidi ya Yemen, akisisitiza kwamba, kutoegemea upande wowote ni sharti la kimsingi kwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake.
Ndege za kivita za Saudia zinashambulia kwa mabomu maeneo ya wanaotaka kujitenga huko kusini mwa Yemen wanaoungwa mkono na Muungano wa Falme za Kiarabu huku kukiwa na mvutano mkali kati ya Saudia na Imarati.
Siku chache zilizopita pia, ndege za kivita za Saudi Arabia zilishambulia shehena za silaha zilizopelekwa na Imarati huko Yemen ambazo zilitakiwa kuwafikia wapiganaji wa Baraza la Mpito la Kusini ambalo ni mamluki wa Imarati. Kuna video zilizosambaa mitandaoni zikionesha kwamba vikosi vya Homeland Shield vya mamluki wa Saudia vinasonga mbele kuelekea mji wa Mukalla wa Yemen, na kuteka maeneo mapya huko Hadhramout.