Qalibaf: Waandamanaji wasikilizwe, vibaraka wa mataifa ya kigeni watashughulikiwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135144-qalibaf_waandamanaji_wasikilizwe_vibaraka_wa_mataifa_ya_kigeni_watashughulikiwa
Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema kwamba maandamano ya watu lazima yasikilizwe, huku akionya kwamba watu binafsi wanaohusishwa na mashirika ya ujasusi ya kigeni wanaotaka kuteka nyara maandamano ya amani ya wananchi na kuyageuza kuwa ghasia, lazima washughulikiwe kivyao.
(last modified 2026-01-05T07:53:56+00:00 )
Jan 05, 2026 07:53 UTC
  • Spika Mohammad Baqer Qalibaf
    Spika Mohammad Baqer Qalibaf

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, amesema kwamba maandamano ya watu lazima yasikilizwe, huku akionya kwamba watu binafsi wanaohusishwa na mashirika ya ujasusi ya kigeni wanaotaka kuteka nyara maandamano ya amani ya wananchi na kuyageuza kuwa ghasia, lazima washughulikiwe kivyao.

Akizungumza mapema leo katika kikao cha wazi cha Bunge, Qalibaf amesisitiza kwamba hatua kama hizo ni muhimu ili kuhakikisha kwamba usalama na amani ya watu haiathiriwi.

Maandamano yalizuka wiki iliyopita baada ya wafanyabiashara mjini Tehran kufunga biashara zao kwa muda kupinga kushuka kwa kasi kwa sarafu ya taifa dhidi ya dola ya Marekani.

Maafisa wa Iran wamekiri kuwepo shinikizo la kiuchumi linalowakabili wananchi na kusema maandamano ya amani ni halali. Wakati huo huo, wameonya kwamba watu wanaopewa himaya na madola ya kigeni wanataka kutumia hali hiyo vibaya na kuchochea vurugu na machafuko.

Spika Mohammad Baqer Qalibaf amesema kwamba "taifa la Iran, katika historia yote, limewaweka mamluki, wasaliti na wauzaji wa nchi mahali pao wanapostahiki, na leo pia haitachukua muda mrefu kabla ya adui kushindwa tena mbele ya watu wa Iran, licha ya kutumia vyombo vyake vyote vya ujasusi, hujuma za kiusalama na vyombo vya habari."

Ameeleza kuwa mwongozo wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei kuhusu udharura wa kuwatenganisha waandamanaji na wanaozusha fujo na wachochezi "uko wazi na unatoa funzo," akiuita kuwa ni ramani ya njia ya kudhibiti machafuko.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alionya Jumamosi iliyopita kwamba 'maandamano ya amani ya wananchi' ni halali, lakini maandamano ni tofauti na ghasia," akiongeza kwamba maafisa wa serikali lazima wawasiliane na waandamanaji, kwa sababu "kuzungumza na mwandamanaji ni tofauti na kuzungumza na mfanyafujo; kuzungumza na mfanyafujo hakuna maana, na lazima awekwe mahali pake."