Ubalozi wa Palestina wafunguliwa rasmi jijini London
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135172-ubalozi_wa_palestina_wafunguliwa_rasmi_jijini_london
Ubalozi wa Palestina umefunguliwa rasmi jijini London, takriban miezi minne baada ya Uingereza kutangaza kuitambua Nchi ya Palestina.
(last modified 2026-01-06T07:08:49+00:00 )
Jan 06, 2026 07:08 UTC
  • Ubalozi wa Palestina wafunguliwa rasmi jijini London

Ubalozi wa Palestina umefunguliwa rasmi jijini London, takriban miezi minne baada ya Uingereza kutangaza kuitambua Nchi ya Palestina.

Ubalozi huo, ambao hapo awali ulikuwa ofisi ndogo ya uwakilishi ya Palestina katika eneo la Hammersmith magharibi mwa London, umefunguliwa rasmi Jumatatu mbele ya kundi la wanadiplomasia wa kigeni na mwakilishi wa kidiplomasia wa Uingereza, Alistair Harrison, pamoja na wafuasi wa Palestina.

Akizungumza katika sherehe ya ufunguzi huo, Balozi wa Palestina jijini London, Husam Zomlot alilielezea jengo la ubalozi huo kama "kipande cha Palestina kwenye ardhi ya Uingereza" na "nembo ya amani, uthabiti, heshima, na (matunda) ya juhudi za watu [Wapalestina] za (kupata) haki na uhuru."

Ameliita tukio hilo kuwa "lahadha ya kihistoria" na "hatua kubwa" katika uhusiano wa Uingereza na Palestina, na katika safari ndefu ya watu wa Palestina kuelekea uhuru kamili na kujitawala.

Serikali ya Uingereza, katika hatua ya kihistoria mnamo Septemba 20, 2025, ilitambua Palestina kama taifa huru na yenye mamlaka ya kujitawala, huku Waziri Mkuu, Keir Starmer akitangaza kwamba uamuzi huo umefungua "ukurasa mpya katika uhusiano wa London na Palestina."

Katika hatua nyingine, mamia ya watu wamekusanyika mkabala na mtaa maarufu wa 10 Downing Street jijini London, wakiitaka serikali ya Uingereza kulaani uchokozi wa Marekani dhidi ya Venezuela.

Waandamanaji hao waliokusanyika chini ya kaulimbiu "Achaneni na Venezuela’ pia wametaka kukomeshwa mara moja kwa hatua yoyote ya kijeshi na kurejeshwa kwa Rais aliyetekwa nyara Nicholas Maduro katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini.