Hamas imerejesha nafasi yake kama mtawala wa Ukanda wa Ghaza
-
Hamas yarejesha nafasi yake kama mtawala wa Ukanda wa Ghaza
Shirika la habari la Tasnim limevinukuu vyombo vya habari vya Israel vikitangaza kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imerejesha udhibiti wake kama mtawala mwenye nguvu kwenye Ukanda wa Ghaza.
Vyombo vya habari vya Kizayuni kikiwemo kituo cha televisheni cha Channel 14 cha Israel vimetangaza kuwa, harakati ya Hamas inaendelea kuimarisha nguvu na udhibiti wake ndani ya Ukanda wa Ghaza licha ya kuweko vitisho vya Trump. Aidha harakati hiyo inakataa kukabidhi silaha, na maafisa wake wakuu wanasisitiza kwamba jambo hilo kamwe halitatokea.
Channel 14 ya televisheni ya Israel imedai pia kuwa, shambulio la siku chache nyuma lililofanywa dhidi ya jeshi la Israel ni ukumbusho mwingine wa ukweli mchungu uliopo hivi sasa kwamba Israel imeshindwa kufikia malengo yake ya kuanzisha vita vya zaidi ya miaka miwili vya Ghaza na inathibitisha kwamba Hamas haina nia ya kuweka chini silaha.
Televisheni hiyo ya Israel imesema kwa uchungu kwamba utawala wa Kizayuni umefeli; huku uongozi wa Hamas ukiendelea kutangaza waziwazi na kwa kujiamni kwamba haitoweka chini silaha.
Katika sherehe za kuhitimu idadi kubwa ya wanafunzi wa udaktari wa vyuo vikuu viwili vyenye mfungamano na HAMAS yaani Chuo Kikuu cha Al-Azhar na Chuo Kikuu cha Kiislamu kilichoanzishwa na Sheikh Ahmed Yassin huko Ghaza, HAMAS ilionesha wazi kuwa ndiyo inayotawala Ghaza.
Licha ya kuweko mashambulizi ya kijeshi ya Israel, vitisho vya nje na njama za mamluki waliopangwa na Israel kuishambulia Hamas, lakini harakati hiyo inazidi kuimarika. Mapambano kuhusu mustakabali wa Ukanda wa Ghaza yanaonekana hayajaisha kabisa.