Qalibaf: Israel ilibembeleza kusitisha mapigano wakati wa vita vya siku 12
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135184-qalibaf_israel_ilibembeleza_kusitisha_mapigano_wakati_wa_vita_vya_siku_12
Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa: Katika siku chache za mwisho za vita vya siku 12, utawala wa Kizayuni uliomba kwa kubembeleza kusitisha mapigano na ukweli huo unaonesha nguvu ya Muqawama wa taifa la Iran mbele ya wavamizi.
(last modified 2026-01-06T08:41:44+00:00 )
Jan 06, 2026 08:41 UTC
  • Qalibaf: Israel ilibembeleza kusitisha mapigano wakati wa vita vya siku 12

Spika wa Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa: Katika siku chache za mwisho za vita vya siku 12, utawala wa Kizayuni uliomba kwa kubembeleza kusitisha mapigano na ukweli huo unaonesha nguvu ya Muqawama wa taifa la Iran mbele ya wavamizi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Mohammad Baqer Qalibaf amesema hayo alipokuwa anahutubia mkutano wa jumuiya ya wafanyakazi na uzalishaji kuhusu fikra ya kufa shahidi na mapambano na kusema: Kufa shahidi si tukio la bahati nasibu, bali ni matunda ya kazi ya kihikma, uwajibikaji, na muono wa mbali. Njia hii ni chaguo la kuwa na welewa wa kina baina ya kuishi kwa raha na kuishi katika mapambano magumu kwenye njia ya matukufu ya Mwenyezi Mungu na ya kibinadamu.

Aidha amesema: Kabla ya mtu kufikia hadhi na daraja ya kufa shahidi, huwa ameshinda kwenye jihadi ya nafsi na kudhibiti matamanio ya nafsi na huwa ameingia katika maisha ya kujitolea kwa ajili ya kupigania haki na kukabiliana na ubeberu na ukandamizaji. Ni sawa kabisa na alivyokuwa anasisitiza Shahid Soleimani kwamba, kabla ya mtu kupanda daraja na kufikia hadhi ya kufa shahidi, lazima mtu huyo awe shahidi kwanza katika maisha yake ya kimwili.

Spika wa Bunge la Iran ameendelea kusema kuwa, katika siku chache za mwisho za vita vya siku 12, utawala wa Kizayuni ulikuwa unaomba kwa kubembeleza kusitisha mapigano. Ukweli huo unaonesha nguvu za Muqawama wa taifa la Iran dhidi ya wavamizi. Qalibaf amesisitiza kuwa, lazima tudumishe mbinu na njia tuliyofuata katika Vita vya Kujihami Kutakatifu na uzoefu wa Kambi ya Muqawama.

Tuliona siku za vita vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi yetu, uzoefu huo ulitufundisha kwamba uvumilivu na Muqawama ndiyo njia pekee ya kutetea maadili na matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu.