Iran: Marekani lazima imwachie huru Rais iliyemteka nyara wa Venezuela
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135146-iran_marekani_lazima_imwachie_huru_rais_iliyemteka_nyara_wa_venezuela
Iran, kwa mara nyingine tena, imekosoa kitendo cha Marekani cha kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flore, na kueleza kuwa waliotekwa nyara lazima waachiwe huru kama inavyosisitizwa na maafisa na wananchi wa Venezuela.
(last modified 2026-01-05T08:04:14+00:00 )
Jan 05, 2026 08:04 UTC
  • Iran: Marekani lazima imwachie huru Rais iliyemteka nyara wa Venezuela

Iran, kwa mara nyingine tena, imekosoa kitendo cha Marekani cha kumteka nyara Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flore, na kueleza kuwa waliotekwa nyara lazima waachiwe huru kama inavyosisitizwa na maafisa na wananchi wa Venezuela.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baqaei amesema leo katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari mjini Tehran kuwa tukio lililojiri Venezuela lilikuwa "hatari sana" na limekosolewa na kulaaniwa vikali  na nchi nyingi duniani.

"Kimsingi, hakuna nchi inayowajibika na yenye mamlaka halali ya kujitawala inayoweza kubakia kimya mbele ya yaliyojiri Venezuela bila kujali ni nani anayeathiriwa au ni katika nchi gani yamefanyika," amesema Esmail Baqaei. Amesisitiza kuwa hatua ya kukiuka mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi wa nchi huru haiwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile, na ni kinyume na misingi yote ya sheria za kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la  Usalama la umoja huo wana jukumu la moja kwa moja la kulinda kanuni na malengo ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Wanajeshi wa Marekani juzi Jumamosi walimteka nyara Rais Nicolas Maduro na mkewe, Cilia Flore huko Caracas mji mkuu wa Venezuela na kuwasafirisha hadi New York, Marekani katika mashambulizi makaliya kijeshi yaliyohusisha ndege na meli za kivita na makomandoo wa Marekani.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran juzi jioni alizungumza kwa simu na waziri mwenzake wa Venezuela, Yvan Gil Pinto na kulaani vikali mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo na kutekwa nyara rais wa nchi na mkewe. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameitaja hatua hiyo ya Marekani kuwa ugaidi wa kiserikali na kulitaka Baraza la Usalama la UN kusitisha hujuma za Marekani dhidi ya Venezuela.