Iran, Cuba, Brazil zataka kuheshimwa sheria za kimataifa
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Cuba na Brazil wamesisitiza udharura wa kuwepo ushirikiano wa karibu na uratibu miongoni mwa nchi zinazostawi katika majukwaa ya kimataifa, ili kukabiliana na mfumo wa ubeberu; na kuunga mkono sheria za kimataifa na kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na mwenzake wa Brazil Mauro Vieira wamefanya mazungumzo ya simu na kusisitizia haja ya mataifa kuungana ili kuzima mwenendo wa kujichukulia maamuzi wa upande mmoja, na kutaka kuheshimiwa sheria za kimataifa.
Akirejelea shambulio la kijeshi la Marekani dhidi ya Venezuela na utekaji nyara wa Rais wa Venezuela, na mkewe, Araghchi amelaani kitendo hicho na kukieleza kama ukiukaji mkubwa wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni za msingi za sheria za kimataifa.
Huku akiunga mkono msimamo huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Brazil amesema kitendo cha Marekani cha kumteka nyara rais wa nchi huru ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na kutangaza kwamba, suala hili litafuatiliwa katika majukwaa ya Baraza la Usalama, Shirika la Mataifa ya Amerika (OAS), na Jumuiya ya Mataifa ya Amerika Kusini na Caribbean (CELAC).
Wakati huo huo, Sayyid Araghchi ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kusimama kidete dhidi ya uvunjaji wa sheria wa Marekani na uchokozi dhidi ya taifa huru la Venezuela. Akizungumza katika mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bruno Rodríguez jioni ya jana Jumatatu, Araghchi aliwasifu watu wa Cuba na serikali kwa ustahimilivu wao thabiti dhidi ya "vikwazo haramu vya kiuchumi na vitisho vya kigeni."
Kwa upande wake, Rodríguez amelaani vitendo vya Washington vya kuvuruga utulivu katika eneo la Caribbean na Amerika Kusini, hasa akishutumu chokochoko haramu dhidi ya Venezuela na kutekwa nyara kwa Rais Nicolas Maduro na mkewe.