"Marubani 30 wa Israel waliuawa katika operesheni ya kulipiza kisasi ya Iran"
Balozi wa zamani wa Iran nchini Iraq amefichua kuwa, marubani 30 wa Israel waliuawa wakati wa moja ya operesheni za kulipiza kisasi za Iran katika vita vya siku 12, akisisitiza kuwa hili lilikuwa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni.
Hassan Kazemi Qomi, balozi wa zamani wa Iran nchini Iraq, amesema katika mahojiano ya televisheni kwamba, katika moja ya operesheni za Iran wakati wa vita vya siku 12, marubani 30 wa Israel waliuawa. "Hili si jambo dogo kwa utawala wa [Israel]," ameeleza hayo na kuongeza kwamba, maelezo mengi kuhusiana na operesheni hizo yamefichwa na utawala wa Tel Aviv hadi sasa.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesisitiza kuwa, lengo kuu la adui ni kubadilisha mfumo wa utawala nchini Iran na kurejea Marekani katika Jamhuri ya Kiislamu, lakini "wameshindwa kufikia malengo yao."
Kazemi Qomi amesisitiza kuwa, jeshi la Iran chini ya uongozi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, lilitoa pigo kubwa kwa Israel, na kukwamisha ajenda pana za adui katika eneo.
Wakati utawala wa Kizayuni ukiendesha vita vya kichokozi dhidi ya Iran tarehe 13 Juni na kuyashambulia maeneo ya kijeshi, nyuklia na makaazi ya Iran kwa muda wa siku 12, Marekani iliingilia kati na kufanya mashambulizi ya kijeshi katika maeneo matatu ya nyuklia huko Natanz, Fordow na Isfahan ya Iran tarehe 22 Juni.
Vikosi vya jeshi la Iran vilifanya mashambulizi makali mara baada ya uvamizi huo. Kikosi cha Wanaanga cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kilitekeleza mawimbi 22 ya hujuma za makombora kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni ikiwa ni sehemu ya Operesheni ya Ahadi ya Tatu ya Kweli ambayo iliisababishia hasara kubwa miji katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Aidha Jeshi la Iran lilitungua ndege kadhaa za kivita aina ya F-35 za utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kutumia mifumo ya ulinzi wa anga iliyotengenezwa ndani ya Iran wakati wa vita hivyo.