Madaktari Wasio na Mipaka: Wafanyakazi wetu waliuawa kwa makusudi Tigray
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema wafanyakazi wake watatu "waliuawa kwa makusudi" wakati wa mapigano makali katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.
Shirika hilo linalojulikana kama MSF jana Jumanne lilichapisha matokeo ya mapitio yake ya ndani kuhusu mauaji ya wahudumu wake hao wakati mapigano yaliposhtadi katika eneo hilo mwaka 2021 na kusema kuwa, wahudumu wake waliouawa kwa makusudi ni Maria Hernandez, raia wa Uhispania, na Waethiopia Yohannes Halefom Reda na Tedros Gebremariam Gebremichael.
Mkoa wa kaskazini wa Tigray ulikuwa uwanja wa vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe, hasa baina ya waasi wa TPLF na vikosi vya serikali ya shirikisho baina ya mwaka 2020 na 2022, vita ambavyo viliua watu wapatao 600,000. Mzozo huo ulisababisha pia maafa ya kibinadamu, na kuacha watu zaid ya milioni moja bila makazi, huku makubaliano dhaifu ya amani yakisababisha mpasuko mkubwa.
MSF imeishutumu serikali ya Ethiopia kwa kushindwa "kutekeleza wajibu wake wa kimaadili" kukamilisha uchunguzi wa mauaji hayo. "Uhakiki huo ulithibitisha kwamba shambulio hilo yalikuwa mauaji ya kukusudia na yaliyolenga wafanyakazi watatu waliotambuliwa wazi," imesema taarifa ya MSF.
Haya yanajiri huku Gavana wa Tigray kwa upande wake akionya kuwa, eneo hilo lingali linakabiliwa na mzozo mbaya wa kibinadamu kutokana na kuvurugwa juhudi za kuwarudisha watu waliokimbia makazi yao na migogoro ya ndani ambayo inayumbisha utulivu.
Wiki chache zilizopita, Umoja wa Afrika (AU) ulielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu matukio yanayojiri katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, ambapo mizozo ya kisiasa kati ya pande zinazohasimiana inatishia makubaliano tete ya amani yaliyomaliza vita katika eneo hilo.