Baghaei: Israel ibebeshwe dhima kwa mashambulizi ya kinyama Lebanon
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiwajibisha Israel kwa uhalifu wa kivita, kufuatia wimbi la mashambulizi mabaya dhidi ya Lebanon, na kukanyaga makubaliano ya kusitisha mapigano.
Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali mashambulizi ya anga ya Wazayuni yaliyolenga miundombinu ya makazi, viwanda, na miji huko kusini mwa Lebanon na Bonde la Bekaa.
Baghaei ameyataja mashambulizi hayo kama "ukiukwaji mkubwa wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa." Amesisitiza umuhimu wa kuushtaki na kuuwajibisha utawala wa Kizayuni kwa kufanya uhalifu huo wa kivita.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameutaka Umoja wa Mataifa na nchi za kikanda kuchukua "hatua kali" ili kukabiliana na uchokozi huo wa utawala vamizi wa Israel.
Israel imefanya mfululizo wa mashambulizi ya anga katika maeneo yote ya kusini na mashariki mwa Lebanon, ikiendelea kukanyaga makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo lengo lake ni kukomesha uchokozi na uvamizi wa Tel Aviv dhidi ya uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi hiyo ya Kiarabu.
Mashambulizi hayo yaliyofanyika kwenye miji ya al-Manara katika eneo la Bekaa na wilaya ya Jezzine kusini mwa Lebanon mbali na kupelekea watu kadhaa kuuawa, lakini yamezilazimisha familia nyingi kuhama maeneo hayo.
Siku ya Jumapili, Israel ilishambulia gari katika eneo la Ayn al-Mizrab, kaskazini mwa mji wa Bint Jbeil huko kusini mwa Lebanon na kuua watu wawili. Hujuma hizo zilijeruhi watu wengi kadhaa katika maeneo tofauti ya Lebanon Jumatatu na jana Jumanne.