Marekani ilidhani Maduro wa Venezuela ni Noriega, ikapata Mandela
Ubalozi wa Jamhuri ya Bolivaria ya Venezuela ulioko Tehran, mji mkuu wa Iran, umefananishia Rais Nicolas Maduro , aliyetekwa hivi karibuni , na kiongozi wa kupinga ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini, shujaa Nelson Mandela, ukisisitiza kuwa Marekani imekosea kutathmini uongozi wa Venezuela na wananchi wake.
Katika ujumbe ulioshirikishwa sambamba na picha za Maduro na Mandela, ubalozi ulisema kuwa Marekani ilitarajia kukutana na kiongozi wa mtindo wa Manuel Noriega wa Panama, lakini badala yake ikakutana na hali yenye athari sawa na ile ya Mandela. Ubalozi wa Venezuela umeandika: “Walidhani wanakabiliana na Manuel Noriega, lakini hatima ikawaletea Mandela.”
Taarifa hiyo pia ilisema kuwa Marekani imeshindwa kuelewa itikadi ya “Chavista” ya Venezuela na msimamo thabiti wa wananchi wake. Marejeo ya Noriega yalihusiana na muktadha wa kihistoria wa uvamizi wa Marekani nchini Panama mnamo Desemba 1989, ambapo Noriega alikamatwa na baadaye akakabiliwa na kesi nchini Marekani.
Ulinganisho huo kati ya Maduro na Mandela unalenga kuonyesha simulizi ya Venezuela kuhusu upinzani wa kisiasa, mapambano na ustahimilivu, ukimuweka kiongozi huyo aliyetekwa kama alama ya kupinga ubeberu wa Marekani badala ya kufuata mkondo wa Noriega.
Maduro na mkewe walitekwa na jeshi vamizi la Marekani kutoka makazi yao mjini Caracas Jumamosi, wakasafirishwa kwa helikopta na kisha kwa meli ya kivita umbali wa takribani kilomita 3,400 hadi New York City, ambako wanakabiliwa na mashtaka ya shirikisho. Hatua hiyo ya ugaidi wa kiserikali ilihitimisha miezi ya shinikizo na maandalizi ya kijeshi katika pwani ya Venezuela, ikiwemo mashambulizi kadhaa dhidi ya meli zilizodaiwa kubeba dawa za kulevya, yaliyosababisha vifo vya angalau watu 115 , operesheni ambazo Caracas imezitaja kuwa za kubuni.
Serikali ya Venezuela imekanusha mara kwa mara kuhusika na biashara ya dawa za kulevya, ikisisitiza kuwa Washington imetumia madai hayo kuhalalisha uvamizi haramu uliolenga kuipindua serikali na kutwaa utajiri mkubwa wa madini na mafuta katika taifa hilo. Saa chache baada ya shambulio hilo, Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa Marekani itaendesha Venezuela kwa muda na itahusika “kwa nguvu kubwa” katika sekta ya mafuta, kauli zilizothibitisha madai ya Venezuela kuhusu malengo halisi ya Washington.
Kutekwa kwa Maduro kulijadiliwa katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo nchi nyingi washiriki zililaani hatua ya Marekani kama kinyume na sheria za kimataifa. Iran, Russia na China pia zimelaani operesheni hiyo na zimeitaka Marekani imeachilie huru Maduro mara moja.