Hizbullah: Israel haiwezi kamwe kufikia malengo yake katika medani ya vita
-
Sheikh Na'im Qassem
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, ameashiria "kugonga mwamba wa mradi wa Israel," na kusisitiza kwamba, utawala huu hautaweza kamwe kufikia malengo yake katika medani ya vita.
Sheikh Na'im Qassem, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbollah ya Lebanon, amesema hayo katika kumbukumbu ya Ashura na kubainisha kwamba, "Tuko katika hatua mpya katika historia ya Lebanon, muqawama, jeshi na taifa. Kwa sasa tuko katika hatua inayoitwa ksambaratisha mpango wa Israel."
Sheikh Naim Qassem amesema: Njia pekee ya kuikomboa ardhi ya Lebanon, kupata uhuru na mamlaka, ni kupinga ukoloni, na kinachohitajika ni jeshi, watu, muqawama na wananchi wote kushirikiana na muqawama.
Katibu Mkuu wa Hizbullah aliendelea kusema, kutokana na uratibu mpana kati ya Marekani na utawala wa Kizayuni imeonekana wazi kwamba, kuna makubaliano na uratibu kati ya Washington na Tel Aviv. Kwetu sisi, hakuna dhamana nyingine isipokuwa nguvu zetu wenyewe. Nguvu zetu ni muqawama uliojengwa juu ya imani, nia na uwezo. Tumesubiri kwa miezi 15, na uvumilivu umekuwa sehemu muhimu ya uwanja wa vita. Usidhani uvumilivu ni kujiondoa na kulegeza msimamo.
Naim Qassem aliongeza: Tuliiingia vitani kwa msaada na uungaji mkono wa Iran, na tukaboresha uwezo wetu wenyewe. Tunaishukuru Iran na kuwambia kuwa wao ndio wenye heshima zaidi duniani. Tuliweza kufikia hatua hii, na wakati, uchaguzi, vita, na hatua zote zilikuwa muhimu sana. Kile ambacho sasa kimetokea ni kusitishwa mapigano, kukiambatana na kujiondoa Israel kutoka Lebanon. Uondoaji lazima ufanyike kulingana na ratiba, na Israel haina chaguo ila kuondoka kutoka ardhi ya Lebanon.