Baraza la Seneti Zimbabwe larefusha muhula wa urais
-
Rais Emmerson Mnangagwa
Baraza la Seneti nchini Zimbabwe limeidhinisha kwa wingi mkubwa wa kura marekebisho ya katiba yenye utata ambayo yatamfanya Rais Emmerson Mnangagwa kubakia madarakani hadi mwaka 2030.
Hatua hiyo inayolalamikiwa na mrengo wa upinzani inayapa mabadiliko hayo uungwaji mkono kamili wa bunge baada ya kuidhinishwa awali na bunge la taifa.
Muswada huo sasa lazima utiwe saini na Rais Emmerson Mnangagwa ili upitishwe kuwa sheria. Rais wa Seneti Mabel Chinomona alisema maseneta 75 walipiga kura ya kuunga mkono na wanne wakaupinga.
Katika bunge la taifa mnamo Juni 18, wabunge 216 walipiga kura ya kuunga mkono na 42 wakaupinga.
Mabadiliko hayo makubwa -- yaliyotajwa na wakosoaji kuwa "mapinduzi ya kikatiba" -- yanajumuisha kifungu ambacho kinaongeza mihula ya urais na ubunge kutoka miaka mitano hadi saba.
Hii ina maana kwamba muhula wa mwisho kati ya miwili ya Mnangagwa inayoruhusiwa kikatiba utaongezwa hadi 2030.
Aidha marekebisho mengine yanalipa bunge mamlaka ya kumteua rais, na kuondoa uchaguzi wa moja kwa moja wa rais ulioanzishwa mwaka 1987, miaka saba baada ya uhuru wa Zimbabwe.
Wakosoaji wanasema kuwa, marekebisho hayo yataimarisha udhibiti wa chama tawala cha Zanu-PF, ambacho kimetawala nchi hiyo yenye utajiri wa rasilimali tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1980. Mnangagwa aliingia madarakani mwaka wa 2017 katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi yaliyomng'oa madarakani Robert Mugabe ambaye alikuwa rais wa nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 30.