Je, Greenland ni Venezuela inayofuata?
Waziri Mkuu wa Denmark amepinga madai mapya ya Donald Trump kuhusu kuimiliki eneo la Greenland na kuitaka Washington ikome kutoa vutisho dhidi ya mshirika wake huyo wa kihistoria.
Bila kupepesa macho na akizungumza waziwazi, Mette Frederiksen ameyataja madai ya sasa ya Donald Trump kuhusu "kuimiliki Greenland" kuwa ya kipuuzi kabisa.
Msimamo huo mkali unadhihirisha wasiwasi mkubwa wa Copenhagen na miji mikuu mingine ya Ulaya kuhusu mabadiliko ya msingi katika mwenendo wa kistratejia wa Marekani. Mabadiliko hayo yameambatana na wasiwasi mkubwa hasa baada operesheni ya kijeshi ya Marekani nchini Venezuela na kutekwa nyara rais wa nchi hiyo.
Madai ya Trump kuhusu Greenland si jambo jipya. Wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais, Trump alitamka mara kadhaa kuhusu "kununua" au kukinyakua kisiwa hicho cha Denmark chenye mamlaka ya ndani . Hata hivyo tofauti na mazingira sasa ni kwamba, mara hii, matamshi haya yametolewa katika hali ambayo Marekani imeonyesha kivitendo kuwa iko tayari kufanya uuvamizi wa kijeshi wa moja kwa moja na kukiuka wazi mamlaka ya kujitawala ya nchi balimbali ili kufikia malengo yake ya kijiopolitiki. Oparesheni ya kijeshi iliyofanywa na Marekani huko Caracas na kumteka nyara Nicolas Maduro, kwa mtazamo wa nchi za Ulaya imebadili mstari mwekundu katika sera za kimataifa; na jambo hili imenyanyua juu vitisho vya Trump dhidi ya Greenland kutoka kiwango cha kuwa "kauli zenye utata" hadi kiwango cha "jambo linalowezekana."
Msimamo mkali wa serikali ya Denmark dhidi ya matamshi ya Trump unaeleweka vyema katika muktadha huo. Frederiksen amesisitiza kuwa ni jambo lisilotasawarika Marekani kuidhibiti Greenland na ametetea mamlaka ya kitaifa ya Denmark. Waziri Mkuu wa Denmark amezungumzia pia sheria za kimataifa na kanuni ya kutobadilisha mipaka kwa kutumia mabavu. Msimamo huu umedhihirisha wasiwasi mkubwa wa nchi za Ulaya kuhusu nia ya Marekani. Wasiwasi kuhusu kurejea mantiki ya kibeberu ya madola makubwa na kudhoofika sheria ambazo zimeunda msingi wa usalama wa bara Ulaya baada ya Vita Vikuu vya Pili ya Dunia.
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Greenland, Jens Frederik Nielsen ameutaja ujumbe wa mke wa afisa wa ngazi ya juu wa Ikulu ya Rais Marekani (White House), ambaye alichapisha ramani ya eneo hilo ikiwa na rangi za bendera ya Marekani kuwa ni "utovu wa heshima" wa waziwazi na kusisitiza kuwa mustakabali wa Greenland hautaamuliwa kupitia jumbe za mitandao ya kijamii. Msimamo huu unaonyesha hisia kali za watu wa Greenland dhidi ya hatua yoyote ya kupuuza nafasi ya kisheria na kisiasa ya ardhi hiyo ambayo ingawa ndogo kwa idadi ya watu, lakini imekuwa kitovu cha ushindani kati ya mataifa makubwa kutokana na eneo lake la kijiopolitiki na rasilimali zake muhimu za madini.
Msimamo huo umevuka mipaka ya Denmark na kuingia katika nchi nyingine za Ulaya. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametuma ujumbe wa wazi kwa Washington akisisitiza uungaji mkono wake usioyumba kwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya Denmark. Amesema: Ulaya haitakaa kimya mbele ya vitisho vya kubadili mipaka ya bara hilo. Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya pia ametangaza mshikamamo wake na Denmark na wananchi wa Greenland na kusema mashauriano yanaendelea na waitifaki wao. Huu ni msemo wa kidiplomasia unaoakisi juhudii za Ulaya za kutafuta jibu la pamoja kwa sera zisizotabirika za Marekani.
Kinachoitia wasiwasi Ulaya si kadhia ya Greenland pekee, bali suala kuu ni kigezo cha mwenendo mpya wa jinsi ya kukabiliana na nchi mshirika wa jadi wa Ulaya, ambayo sasa imekuwa sababu ya kuteteresha na kuvuruga amani ya duniani. Kama Venezuela iinashambuliwa kijeshi kwa misingi ya maslahi ya kiusalama au kiuchumi, kuna dhamana gani kwamba mantiki kama hiyo haitatumika dhidi ya maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na ncha ya kaskazini? Hili ni swali ambalo sasa linaibuliwa katika vyumba vya fikra vya Ulaya.
Na mwisho, jibu au radiamali ya serikali ya Denmark na nchi nyingine za Ulaya kwa madai ya Trump kuhusu Greenland zaidi ya kuwa hatua ya kutetea mamlaka ya eneo moja, ni jitihada za kuhami kanuni kuu za mfumo wa kimataifa. Nchi za Ulaya zimeelewa vyema kwamba kukaa kimya mbele ya madai kama haya ya Trump kunaweza kufungua njia ya kuhalalisha sera za utumiaji mabavu katika siasa za kiimataifa.