Imarati inapanga kuijengea Israel kambi ya jeshi karibu na Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i135212-imarati_inapanga_kuijengea_israel_kambi_ya_jeshi_karibu_na_saudi_arabia
Vyombo vya habari vya Saudi Arabia vimefichua mpango wa Umoja wa Falme za Kiarabu wa kujenga kambi ya kijeshi ya Israel karibu na mpaka wa nchi hizi mbili za Kiarabu.
(last modified 2026-01-07T10:13:18+00:00 )
Jan 07, 2026 10:13 UTC
  • Imarati inapanga kuijengea Israel kambi ya jeshi karibu na Saudi Arabia

Vyombo vya habari vya Saudi Arabia vimefichua mpango wa Umoja wa Falme za Kiarabu wa kujenga kambi ya kijeshi ya Israel karibu na mpaka wa nchi hizi mbili za Kiarabu.

Vyombo vya habari vya Saudia vimeripoti kwamba, UAE inataka kujenga kambi ya kijeshi ya Israel katika eneo la Arada, lililoko karibu na mpaka wa pamoja na Saudi Arabia. Haya yanajiri huku ndege za kivita za Saudia zikiendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya mamluki wa Imarati yakiwemo makao makuu ya mamluki hao huko mashariki mwa Yemen.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kambi hiyo itakuwa makazi kwa wanajeshi 800 wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Habari zaidi zinasema kuwa, hatua hii ya UAE inachukuliwa kwa shabaha ya kuimarisha ushirikiano na utawala wa Tel Aviv.

Inaarifiwa kuwa, hati za siri zinazohusishwa na Shirika la Ujasusi la UAE zilifichua kiwango cha ushirikiano wa kijasusi kati ya serikali ya Imarati na Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad), zikiwemo operesheni za ujasusi ndani ya Ukanda wa Gaza na Qatar, na utekelezaji wa maagizo ya moja kwa moja kutoka kwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Mwezi Juni mwaka 2021, Imarati ilifungua rasmi ubalozi wake mjini Tel Aviv, siku chache tu baada ya dunia kushuhudia jinai na mauaji ya kutisha ya zaidi ya Wapalestina 250 wa Ukanda wa Gaza, yaliyofanywa na jeshi katili la Israel. 

Miezi michache kabla ya hapo, UAE ilianzisha uhusiano rasmi na utawala wa Kizayuni wa Israel, ikawa nchi ya kwanza ya Kiarabu kufanya hivyo baada ya kipindi cha miaka 26. Tawala za Kiarabu kama Sudan, Bahrain na Morocco zilifuata kibubusa mkumbo huo uliolaaniwa si tu na wananchi wao, bali na dunia nzima.

Saudi Arabia na Imarati zimekuwa katika mvutano mkubwa katika miezi ya hivi karibuni. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, Wizara ya Ulinzi ya Imarati ilitangaza kwamba imeamua kujiondoa kijeshi nchini Yemen baada ya ndege za kivita za Saudia kushambulia mamluki wa Imarati kwenye bandari ya Mukalla ya Yemen.