Meja Jenerali Hatami: Vitisho vya maadui havitapita bila kujibiwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135218-meja_jenerali_hatami_vitisho_vya_maadui_havitapita_bila_kujibiwa
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami amesema Jamhuri ya Kiislamu inayatazama matamshi ya vitisho na kichochezi ya maadui zake kuwa tishio la moja kwa moja dhidi ya taifa hili, na itatoa majibu madhubiti iwapo vitisho hivyo vitaendelea kutolewa.
(last modified 2026-01-07T08:02:58+00:00 )
Jan 07, 2026 08:02 UTC
  • Meja Jenerali Hatami: Vitisho vya maadui havitapita bila kujibiwa

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran, Meja Jenerali Amir Hatami amesema Jamhuri ya Kiislamu inayatazama matamshi ya vitisho na kichochezi ya maadui zake kuwa tishio la moja kwa moja dhidi ya taifa hili, na itatoa majibu madhubiti iwapo vitisho hivyo vitaendelea kutolewa.

Meja Jenerali Amir Hatami ameyasema hayo alipokuwa akihutubia makada katika Chuo Kikuu cha Kamandi ya Jeshi hapa mjini Tehran leo Jumatano na kubainisha kuwa, "Vitisho vya maadui havitapita bila kujibiwa."

Jenerali Hatami ameonya kwamba, mahesabu yoyote ghalati ya maadui wa Iran yatakabiliwa na majibu makali zaidi kuliko lile lililotolewa wakati wa vita vya kichokozi vya siku 12, vilivyoanzishwa na Israel na baadaye Marekani dhidi ya Iran.

Akizungumzia maandamano ya karibuni nchini Iran kuhusu hali ya uchumi, Meja Jenerali Hatami amesema maadui wametumia vibaya maandamano hayo kwa lengo la kuchochea machafuko ndani ya nchi.

"Maandamano ni jambo la kawaida na la asili katika nchi yoyote. Jambo lisilo la kawaida, hata hivyo, ni kuyageuza maandamano kuwa machafuko katika muda mfupi sana. Hii ni mbali na tabia ya watu wa Iran na, bila shaka, imekuwa ikipangwa na maadui," amesema.

Kamanda Hatami amesisitiza kuwa, "Tuko macho na tunafuatilia kwa karibu nyendo na harakati zote za adui na tutatoa jibu kali kwa uvamizi wa aina yoyote." Meja Jenerali Hatami ameeleza kuwa, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, likiwa na azma thabiti, limeandaa kila kitu kinachohitajika kukabiliana na maadui zake. 

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Iran ameongeza kwa kusema: Jukumu la jeshi ni kulinda umoja wa kijiografia wa Iran ya Kiislamu na uhuru wa nchi, na sote tunajitahidi kutekeleza jukumu hili kwa njia bora zaidi.