Mvua, mafuriko yaua na kujeruhi makumi ya watu Madagascar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135214-mvua_mafuriko_yaua_na_kujeruhi_makumi_ya_watu_madagascar
Wau wasiopungua 11 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na athari za mvua kubwa ambazo zimekuwa zikinyesha nchini Madagacar kwa wiki kadhaa sasa.
(last modified 2026-01-07T10:16:22+00:00 )
Jan 07, 2026 10:16 UTC
  • Mvua, mafuriko yaua na kujeruhi makumi ya watu Madagascar

Wau wasiopungua 11 wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na athari za mvua kubwa ambazo zimekuwa zikinyesha nchini Madagacar kwa wiki kadhaa sasa.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana Jumanne na Shirika la Kusimamia Majanga nchini humo ambalo limeeleza kuwa, makumi ya watu wamejeruhiwa pia kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo.

Mji mkuu, Antananarivo, ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko hayo. Watu wasiopungua 274 wameathiriwa na mvua hizo, huku nyumba 26 zikiharibiwa au kusombwa kabisa na maji ya mafuriko hayo, imesema Ofisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Dharura na Maafa.

Baraza la Jiji la Antananarivo limewataka wakazi wa mji huo kuendelea kuwa macho, na kutoa wito kwa familia zote zinazoishi katika nyumba za zamani au zisizo salama kuhama na kwenda maeneo salama.

Idara ya Hali ya Hewa ya Madagascar imesema kwamba, mvua zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi, na nyanda za juu eneo la kati katika siku zijazo, huku mvua zikitazamiwa pia katika maeneo ya kusini.

Madagascar ambayo iko magharibi mwa Bahari ya Hindi, kwa kawaida hushuhudia msimu wa mvua za masika kuanzia mwezi Novemba hadi Machi.  Athari za hali hii ya hewa mara nyingi husababisha vifo, watu kuhama makazi yao, na mafuriko katika sehemu kubwa ya ardhi ya kilimo katika kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa Afrika.