Mahakama Kuu ya Katiba ya Madagascar yapinga kuondolewa madarakani Rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138734-mahakama_kuu_ya_katiba_ya_madagascar_yapinga_kuondolewa_madarakani_rais
Mahakama Kuu ya Katiba ya Madagascar imepinga jaribio la mbunge wa upinzani la kumwondoa madarakani Rais Michael Randrianirina wa nchi hiyo.
(last modified 2026-05-30T04:24:21+00:00 )
May 30, 2026 04:13 UTC
  • Rais Michael Randrianirina wa Madagascar
    Rais Michael Randrianirina wa Madagascar

Mahakama Kuu ya Katiba ya Madagascar imepinga jaribio la mbunge wa upinzani la kumwondoa madarakani Rais Michael Randrianirina wa nchi hiyo.

Mbunge mashuhuri Antoine Rajerison alikuwa ameiomba mahakama hiyo kumwondoa mamlakani Kanali Randrianirina akidaiwa kufanya uhaini kwa hatua yake ya "kukiuka pakubwa na mara kwa mara katiba ya Madagascar,”.

Mahakama ya Katiba ya Madagascar iliamua kwamba ombi la mbunge Antoine Rajerison halikubaliki, na kwa kuzingatia kuwa  halikidhi matakwa ya kikatiba ya kumwondoa madarakani mkuu wa nchi.

Kisiwa cha Madagascar bado kipo katika hali tete ya kisiasa huku taifa hilo likijiandaa kuendesha kura ya maoni na uchaguzi wa rais mwaka 2027 kwa mujibu wa ramani ya Randrianirina ya "Kuanzisha Upya Jamhuri".

Randrianirina aliingia madarakani na kuapishwa kuwa Rais wa Madagascar Oktoba mwaka jana, akiongoza serikali ya mpito baada ya wiki kadhaa za maandamano yaliyoongozwa na vijana ambao walipelekea mtangulizi wake, Andry Rajoelina, kuelekea uhamishoni.

Rais wa Madagascar amenusurika kuuawa mara mbili mwanzoni mwa mwaka huu kufuatia kushtadi hitilafu za kisiasa kati ya jeshi na makundi ya kiraia.