Idadi ya waliofariki dunia kutokana na kimbunga nchini Madagascar imefikia 59
Idara yaMaafa ya Majanga ya Kimaumbile ya Madagascar imetangaza kuwa hadi sasa watu 59 wamefariki dunia kutokana na kimbunga cha Gezani kilichoathiri maeneo ya pwani ya mashariki mwa nchi hiyo tarehe 10 mwezi huu huku watu 15 hawajulikani walipo. Wakati huo huo watu zaidi ya 16,000 wamepoteza makazi yao kufuatia kimbunga hicho.
Vifo vingi vimetokea hukoToamasina, jiji la pili kwa ukubwa nchini Madagascar lenye watu 400,000, ambapo kimbunga hicho kilitua na upepo unaofikia kilomita 250 kwa saa.
Uharibifu ni mkubwa ambapo takriban nyumba 25,000 zimeharibiwa, nyumba 27,000 zimejaa maji ya mafuriko na zaidi ya madarasa 200 yamebomoka.
Mji wa Toamasina hivi sasa halina huduma ya maji ya bomba kwa ajili ya wakazi wake unatumia asilimia tano tu ya umeme wake.
Hiki ni kimbunga cha pili kuiathiri Madagascar katika muda wa wiki kadhaasasa kufuatia kimbunga cha kitropiki kwa jina la Fytia, ambacho kiliua takriban watu saba na kupelekea wengine 20,000 kuhama makazi yao mwezi huu wa Februari.
Madagascar ni kati ya nchi ambazo huathiriwa na vimbunga mara kwa mara barani Afrika.
Waziri Mkuu wa Madagascar, Rajaonarivelo Heritsalama, amesema akiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Antananarivo kwamba kimbunga hicho kimeathiri uchumi wa nchi na maisha ya watu na kwamba serikali itajikita katika kuimarisha ustahimilivu ili kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi katika siku zijazo.
Wakati huo huo kimbunga Gezani juzi kilipiga katika mkoa wa pwani ya kusini mwa Msumbiji wa Inhambane, na kuua takriban watu wanne.