IRGC: Iran haiogopi vitisho na haitakubali kutawaliwa na Marekani
Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, amesema kuwa Iran haiogopi vitishio vya maadui na kamwe haitakubali kutawaliwa na Marekani. Ametoa kauli hiyo kujibu vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na Rais wa Marekani Donald Trump.
“Tumelelewa katika madrasa ya mashahidi na hatuogopi adui,” amesema Jenerali Vahidi siku ya Jumane katika kikao na wanajeshi wastaafu wa vita vya Iraq dhidi ya Iran vya miaka ya 1980, kilichofanyika mjini Kerman, kusini mashariki mwa Iran.
Kauli zake zilikuja baada ya Trump kutishia Iran kupitia ujumbe wa mitandao ya kijamii, akidai kuwa Marekani iko “tayari na imejihami” kushambulia Iran. Vitisho hivyo vililaaniwa vikali na Iran, huku maafisa wa Iran wakionya Marekani dhidi ya “chokochoko za kijeshi ya kihasara.”
Vahidi aliongeza: “Mataifa yameanza kutambua kuwa lazima yawe huru na yakatae kutawaliwa na Marekani.” Amebainisha kuwa Washington ipo katika “mkondo wa kuporomoka,” na kwamba nyenzo ilizotumia kutawala dunia zimepoteza nguvu. “Sasa inalazimika kufikia malengo yake kwa kutumia mabavu, vita, ugaidi na uporaji.”
Amesema vitendo kama vile kumteka rais wa taifa au kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani havionyeshi nguvu, bali vinaashiria “kilele cha fedheha na dalili za kuporomoka.” Alikuwa akiashiria tukio la Marekani kumteka Rais wa Venezuela Nicolas Maduro na mkewe, waliosafirishwa hadi New York kwa madai yasiyo na ushahidi ya biashara ya dawa za kulevya.
Jenerali Soleimani, aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC, aliuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani ambalo lilitekelezwa na jeshi la kigaidi la Marekani mjini Baghdad mnamo Januari 2020.
Jenerali Vahidi amesisitiza hadhi ya Soleimani, akisema hakuwa mtu wa kawaida bali, kama alivyoelezwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, alikuwa “madrasa ya fikra” na harakati endelevu inayobaki hai na yenye ushawishi.
Aliongeza kuwa kundi la kigaidi la Daesh iliundwa na maadui wa Iran lakini hatimaye ilishindwa na Shahidi Soleimani, ambaye alikuwa bingwa wa kutatua changamoto ngumu kupitia uongozi, kumtegemea Mwenyezi Mungu na maamuzi ya busara.
Maadui wa Iran walidhani kuwa kumuua Soleimani kungeidhoofisha nchi, lakini badala yake taifa la Iran limekuwa imara zaidi na ushawishi wa Soleimani sasa ni mkubwa kuliko awali, Vahidi alisema.
Naibu Kamanda wa IRGC alihitimisha kwa kusema kuwa uvumilivu wa Iran utahakikisha mustakabali utakuwa wa Uislamu na taifa la Iran.