Uchunguzi wa maoni: Wajapani hawako tayari kuisamehe Marekani
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni nchini Japan unaonyesha kuwa, nusu ya manusura wa mlipuko wa bomu la atomiki nchini humo "hawawezi" kuisamehe Marekani kwa shambulio la bomu la atomiki nchini Japan.
Mnamo Agosti 6, 1945, ndege ya kurusha mabomu ya B-29 ya jeshi la Marekani, ilirusha bomu la atomiki kwenye jiji la Japan la Hiroshima kwa amri ya Rais wa wakati huo Harry Truman. Siku tatu baadaye, Marekani ilirusha bomu la pili la atomiki kwenye mji wa Nagasaki nchini Japan. Kulingana na vyanzo rasmi, takriban watu 220,000 walikufa kutokana na milipuko hii miwili ya atomiki.
Marekani haijawahi kuomba msamaha kwa kutumia mabomu haya. Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi mpya wa Shirika la Habari la Japan la Kyodo, asilimia 45.7 ya manusura wa shambulio la atomiki nchini humo hawako tayari kuisamehe Marekani kwa mashambulizi ya atomiki katika miji ya Hiroshima na Nagasaki.
Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliochapishwa kwenye tovuti ya TRT Global siku ya Jumapili, pia yanaonyesha kuwa, karibu asilimia 70 ya manusura wa mabomu ya atomiki ya Japan wanahofia kuongezeka kwa hatari za nyuklia huku nchi hiyo ikijiandaa kwa kumbukumbu ya mauaji ya Hiroshima na Nagasaki.
Kwa upande mwingine, rais wa sasa Marekani Donald Trump ambaye alishambulia maeneo matatu nchini Iran mwishoni mwa mwezi wa Juni kwa lengo la kuharibu vituo vya nyuklia vya Iran vilivyo vya amani, alisema katika safari yake ya hivi karibuni nchini Uholanzi kuhudhuria mkutano wa NATO: "Sitaki kutumia mfano wa Hiroshima, sitaki kutumia mfano wa Nagasaki, lakini mambo mawili haya kimsingi yalikuwa sawa."
"Ulipuaji huu ulimaliza vita hivyo." Maafisa, manusura wa mabomu ya atomiki, na wanaharakati wa kupinga vita nchini Japan walijibu vikali matamshi yake ya kulinganisha shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na milipuko ya nyuklia ya Hiroshima na Nagasaki, na kuutaja ulinganisho huo kuwa wa kikatili na wa kutojali.